• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:55 AM
Mikakati ya Uhuru kumpiga jeki Raila

Mikakati ya Uhuru kumpiga jeki Raila

NA BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta yumo mbioni kutekeleza mikakati inayolenga kuvutia wapigakura kumchagua mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance Raila Odinga, huku zikisalia siku 17 kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Katika mikakati hiyo, Rais Kenyatta analenga mpiga kura moja kwa moja, hatua ambayo mpinzani mkuu wa Bw Odinga katika uchaguzi mkuu ujao, Naibu Rais William Ruto amehimiza Wakenya kupuuza.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni utoaji wa hati miliki 6 milioni za ardhi kote nchini, kufungua miradi ya maendeleo, kupunguza bei ya unga na kudhibiti bei za mafuta.

Kupanda kwa bei za mafuta kumesababisha bei za bidhaa muhimu, ikiwemo ya unga wa mahindi kupanda na kulemea Wakenya wengi.

Mnamo Jumatano, Rais Kenyatta aliondoa ushuru wa mahindi yanayonunuliwa nje ya nchi na ada za kuyasafirisha kwa reli kutoka Mombasa.

Alisema hatua hii itafanya bei ya unga wa mahindi kuteremka hadi Sh100 kote nchini Kenya.

Hata hivyo, Dkt Ruto na washirika wake wanasema hatua hii inalenga kufurahisha Wakenya ili wampigie kura Bw Odinga ambaye Rais Kenyatta anaunga mkono kuwa mrithi wake.

Mnamo Julai 14, Rais Kenyatta aliingilia kati kwa mara ya kwanza kudhibiti bei za mafuta ambazo zimekuwa zikiongezeka kwa miezi sita iliyopita.

Rais Kenyatta alitangaza serikali ilitoa ruzuku ya Sh14 bilioni kuepusha bei kupanda zaidi.

Siku chache baada ya tangazo hilo, serikali ilichukua hatua za kurudisha uhusiano wa Kenya na Somalia ili kuruhusu zao la miraa kuuzwa katika nchi hiyo jirani baada ya marufuku iliyodumu kwa zaidi ya miaka minne.

Kulingana na wadadisi wa siasa na uchumi, kufunguliwa kwa soko la miraa ni afueni kwa wakazi wa eneo la Mlima Kenya Magharibi ambao wamekuwa wakililia serikali kuwaokoa kiuchumi.

“Kufungua soko la miraa Somalia bila shaka kutafurahisha wapiga kura wa Meru, Embu na Tharaka Nithi ambako Dkt Ruto ana wafuasi wengi,” asema mchambuzi wa siasa Peter Kimotho.

Anasema hatua ambazo Rais Kenyatta amechukua hivi majuzi zinatokana na ripoti za wanamikakakati wa kampeni za Azimio.

Akiwa katika kampeni jijini Nairobi wiki jana, Bw Odinga alikiri kwamba alizungumza na Rais Kenyatta apunguze bei za mafuta na unga.

Mbali na kutoa maagizo kutoka Ikulu, Rais Kenyatta ameanza kuzuru mitaani kumpigia debe Bw Odinga.

Wiki moja iliyopita, rais aliandamana na viongozi wengine Kaunti ya Nairobi kuzuru eneobunge la Embakasi Mashariki kuanzisha zoezi la kutoa hatimiliki za ardhi, ambapo aliwarai wakazi kumpigia kura Bw Odinga Agosti 9.

Rais Kenyatta pia alifungua hospitali ya Mihang’o na pia kutoa vyeti vya ardhi.

Matukio mengine ya hivi karibuni yanaonyesha kiongozi wa nchi ameanza kumtafutia kura mgombea urais huyo wa Azimio ni kuapisha mara moja majaji sita wa Mahakama ya Rufaa ambao waliwasilishwa kwake na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC).

Hii ni tofauti na awali alipokataa kuwaapisha majaji sita walioteuliwa kuhudumu katika mahakama hiyo.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Francis Kebei, rais hakutana kuwapa wapinzani wa Bw Odinga silaha ya kutumia katika kampeni zao.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, hatua za Rais Kenyatta si za kupuuzwa.

“Kuna watu wamenufaika na serikali ya Rais Kenyatta kinyume na dhana ambayo imeendelezwa na wanasiasa wengine. Hivyo, watu hawa watakubaliana naye kwa sababu wanaamini katika utendakazi wake,” alisema Bw Andati.

Wakili Danstan Omari naye anahoji kuwa kampeni za Rais Kenyatta zitampiga jeki Bw Odinga hasa maeneo ya Kati na Kaskazini Mashariki.

“Kampeni za Uhuru pekee zinaweza kumpa Raila zaidi ya asilimia 20 ya kura,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mwanatenisi Okutoyi aanza kuona matunda ya jasho lake,...

Wenyeji Uingereza wapepeta Uhispania na kufuzu kwa...

T L