• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Wenyeji Uingereza wapepeta Uhispania na kufuzu kwa nusu-fainali za Euro za wanawake 2022

Wenyeji Uingereza wapepeta Uhispania na kufuzu kwa nusu-fainali za Euro za wanawake 2022

Na MASHIRIKA

VIPUSA wa Uingereza walifuzu kwa nusu-fainali za Euro 2022 mwaka huu baada ya kutoka nyuma na kukomoa Uhispania 2-1 katika muda wa ziada.

Georgia Stanway alisisimua idadi kubwa ya mashabiki uwanjani Amex Stadium alipofunga bao la ushindi katika dakika ya 96 baada ya warembo hao wa kocha Sarina Wiegman kujikuta wakiwa chini kwa zaidi ya 80.

Awali, Ella Toone alikuwa amesawazishia Uingereza kwa kujaza kimiani krosi ya Alessia Russo ambaye ni mwenzake kambini mwa Manchester United katika dakika ya 84. Esther Gonzalez aliwaweka Uhispania kifua mbele kunako dakika ya 54.

Ushindi wa Uingereza uliwawezesha kutinga nusu-fainali za kipute cha haiba kubwa kwa mara ya nne mfululizo huku wakiendeleza rekodi ya kutopigwa katika msururu wa mechi 18 chini ya kocha Wiegman.

Uingereza kwa sasa ni miongoni mwa vikosi vinavyopigiwa upatu wa kuzoa taji la Euro 2022 kwa mara ya kwanza katika historia. Fainali ya kipute hicho itafanyika Julai 31, 2022. Hata hivyo, watalazimika kwanza kuwapiga kumbo Uswidi au Ubelgiji katika hatua ya nusu-fainali.

Kwa upande wao, Uhispania sasa wameaga kivumbi cha Euro katika hatua ya robo-fainali kwa mara ya tatu mfululizo. Uingereza walishuka dimbani dhidi ya Uhispania wakipigiwa upatu wa kushinda baada ya kukamilisha kampeni zao za makundi kileleni huku wakitamalaki michuano yote mitatu bila kufungwa bao.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mikakati ya Uhuru kumpiga jeki Raila

Afueni kwa Jumwa kesi kuhusu digrii yake ikitupwa

T L