• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Mivutano sasa yatikisa jahazi la Raila Tharaka

Mivutano sasa yatikisa jahazi la Raila Tharaka

NA ALEX NJERU

UHASAMA kati ya vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya ulidhihirika wakati wa ziara ya mgombea mwenza wa Raila Odinga, Martha Karua katika Kaunti ya Tharaka Nithi mnamo Alhamisi.

Bi Karua aliongoza mkutano na viongozi na wananchi katika mji wa Kathwana kuelezea manifesto ya muungano huo na kujibu maswali.

Hata hivyo, ni mgombea ugavana kwa tiketi ya Narc Kenya, Mzalendo Kibunjia, mgombeaji wa useneta kwa tikiti ya Jubilee, Paul Mugambi na madiwani wachache waliohudhuria mkutano huo uliodumu kwa saa kadhaa.

Mgombeaji ugavana kwa tikiti ya Jubilee, Erustus Njoka, mwenzake wa Wiper, Nyamu Kagwima, mgombeaji kiti cha Mwakilishi wa Kike kwa tikiti ya Jubilee, Penninah Kambanja na mwaniaji wa kiti hicho kwa ODM, Saraha Karimi hawakuhudhuria mkutano huo.

Wawaniaji ubunge kwa tikiti ya Jubilee; Dkt Mutegi Kabisani (Tharaka), Mercy Kirito (Chuka/Igambang’ombe) na Lawrence Kaburu (Maara) pia walikwepa mkutano huo.

Bi Karua na Dkt Kibunjia waliwakosoa viongozi hao kwa kudharau mkutano licha ya kwamba walialikwa.

“Viongozi wote wanaowania viti mbalimbali chini ya mwavuli wa Azimio la Umoja One Kenya walialikwa kwa mkutano huo wa mashauriano lakini wakaamua kukaidi mwaliko huo,” akasema Bi Karua.

Kiongozi huyo wa Narc Kenya asikitika kuwa baadhi ya wagombeaji wa viti chini ya Azimio hawajawa wakimfanyia kampeni Bw Odinga. Alisema wanawashauri wakazi kuwapigia kura wagombeaji urais wanaowapenda.

Bw Karua alisema wagombeaji wanaokwepa kumfanyia kampeni Bw Odinga ni walaghai na kwamba hata wakichaguliwa, hawatawahudumia wapigakura ipasavyo.

“Ikiwa kuna mgombeaji ambaye hatampigia debe mgombea urais wake, huyu ni mtu ambaye haungi mkono sera za muungano husika na hafai kuchukuliwa kwa uzito.

Dkt Mzalendo na Bw Mugambe waliwakosoa wenzao kwa kukwepo mkutano huo uliandaliwa kwa ajili ya kufafanua manifesto ya Bw Odinga. Bw Mugambi alisema ili kaunti hiyo ipate mgao mzuri wa mapato ya kitaifa katika serikali ijayo, viongozi wanafaa kuungana na kutetea masilahi ya eneo hilo.

“Nimefika hapa kusikiliza kile kilichoko ndani ya manifesto ya Azimio kwa niaba ya watu wetu ili nikichaguliwa Agosti 9, niweze kufuatilia utekelezaji wake,” akasema Bw Mugambi.

Alipofikiwa kwa njia ya simu, Prof Njoka alikana madai kuwa alialikwa katika mkutano huo na badala yake akamshutumu Dkt Kibunjia kwa kuwaweka “wagombea wengine katika giza”.

Alisema kuwa awali, mkutano huo ulipangiwa kufanyika mjini Chuka lakini baadaye ya Dkt Kibunjia akauhamisha bila kushauriana na viongozi wengine.

“Nilidhani mkutano huo ulikuwa wa Narc-Kenya. Nina mambo mengine ya kufanya hata kama ni kupumzika nyumbani,” Prof Njoka akasema.

Mvutano kati ya wagombeaji viti mbalimbali kwa tiketi za vyama tanzu katika muungano wa Azimio huenda ukachangia ushindi wa wagombea wa Kenya Kwanza katika viti mbalimbali, haswa ugavana, katika kaunti ya Tharaka Nithi.

  • Tags

You can share this post!

ULIMBWENDE: Tumia maziwa kulainisha ngozi yako

TUSIJE TUKASAHAU: Rais alishindwa kabisa kukabili jinamizi...

T L