• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Mkataba wa Musalia, Ruto watatiza Mlima

Mkataba wa Musalia, Ruto watatiza Mlima

MWANGI MUIRURI na LEONARD ONYANGO

MKATABA wa ugavi wa vyeo iwapo Naibu Rais William Ruto atashinda urais katika uchaguzi mkuu ujao umetishia kupunguza ushawishi wa muungano wa Kenya Kwanza katika eneo la Mlima Kenya.

Wakazi wa Mlima Kenya wanasema kuwa mkataba huo uliotiwa saini baina ya Dkt Ruto na kiongozi wa chama cha ANC, Bw Musalia Mudavadi pamoja na kinara wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula, umewasaliti na kuwatenga kimaendeleo.

Kulingana na mkataba huo ambao tayari umepelekwa katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula –wote kutoka eneo la Magharibi – wameahidiwa vinono.

Bw Mudavadi na Wetang’ula wameahidiwa asilimia 30 ya nyadhifa serikalini na kutengenezewa barabara za lami za urefu wa kilomita 1,000 katika ngome yao.

Bw Mudavadi pia atapewa wadhifa wa waziri mkuu pamoja na udhibiti wa wizara ya Usalama inayoshikiliwa kwa sasa na Dkt Fred Matiang’i.

Waziri mkuu atakuwa na mamlaka makubwa kuliko yale ya naibu wa rais ambaye atateuliwa kutoka eneo la Mlima Kenya. Bw Wetang’ula atapewa uspika wa Bunge la Kitaifa.

Gavana wa Kilifi Amason Kingi aliyegura muungano wa Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza ameahidiwa uspika wa Seneti.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi Bw Joseph Kaguthi anashutumu mkataba huo wa Kenya Kwanza huku akidai kuwa umetenga watu wa Mlima Kenya.

“Lengo lake ni kupata kura Mlima Kenya lakini ameashiria kuwatenga watu wa eneo hilo katika serikali yake,” akasema Bw Kaguthi.

Ripoti ya utafiti wa kura ya maoni uliodhaminiwa na kampuni ya Nation Media Group unaonyesha kuwa Dkt Ruto anaungwa mkono kwa asilimia 60 ya wakazi wa eneo la Kati ikilinganishwa na mpinzani wake wa karibu Raila Odinga aliye na asilimia 22.

Kufichuka kwa yaliyomo katika mkataba huo wa Kenya Kwanza huenda kukasababisha asilimia 10 ya wakazi wa Mlima Kenya ambao hawajaamua kuelekeza kura zao katika kapu la Bw Odinga anayeungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo na mbunge wa Gatundu, Bw Moses Kuria tayari wametishia kujiondoa Kenya Kwanza iwapo Dkt Ruto hatawaeleza mgao wa watu wa Mlima Kenya katika serikali yake iwapo atashinda urais.

“Tunataka Ruto kutueleza mgao wetu katika serikali yake. Tunaona tayari Mudavadi na Wetang’ula wametengewa asilimia 30 ya nyadhifa. Ikiwa Ruto hatatueleza mgao wetu tutaondoka Kenya Kwanza. Tukiondoka hata watu 10 katika Kenya Kwanza, ndoto ya Ruto kuwa rais itazima,” akasema Bw Kabogo katika mkutano wa kampeni mjini Thika, Alhamisi.

Kulingana na Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, Dkt Ruto anatarajiwa kukutana na viongozi wa Mlima Kenya kutia saini mkataba wa maelewano kuhusu ugavi wa nyadhifa iwapo Kenya Kwanza itashinda uchaguzi ujao.

Mkataba huo, hata hivyo, hautakubaliwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Ann Nderitu kwani makataa yamepita.

“Mimi ninawazia kujiondoa muungano huu ambao unaanza kutupa ushahidi wa utapeli. Dkt Ruto alikataa tuunge mkono mfumo wa BBI ambao ulikuwa unaunda wadhifa wa waziri mkuu lakini sasa yeye ndiye anauunda hata bila mashauriano na tayari ametunuku wengine nyadhifa nje ya Mlima Kenya. Mswada wa BBI ulikuwa unapendekeza eneo la Mlima Kenya kuongezewa fedha na vyeo kwa kuwa idadi yetu ni kubwa lakini Dkt Ruto aliupinga,” akasema Bw Kabogo.

Bw Kuria alidai kuwa Dkt Ruto ameanza kuonyesha dalili za kutenga eneo la Mlima Kenya hata kabla ya kuchaguliwa rais.

“Ikiwa tunaanza kutengwa mapema hivi, tukiingia serikalini tunaweza tukajipata kwa shida kubwa zaidi na itabidi sasa tukae chini, tuzungumze, tuelewane na tuafikiane jinsi ya kutembea safari hii,” akasema Bw Kuria.

Vyama vingine ambavyo vimeelezea wasiwasi wao na mkataba huo ni vile vya Democratic Party chini ya Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi, The Service Party cha Mwangi Kiunjuri pamoja na Farmners Party cha Irungu Nyakera.

BARAKA

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth ambaye ni mmoja wa viongozi wa Azimio kutoka eneo la Mlima Kenya alisema kuwa kufichuka kwa mkataba huo huenda ikawa baraka kwa Bw Odinga.

“Kufichuka kwa mkataba huo wa Kenya Kwanza kutatoa fursa kwa wakazi wa Mlima Kenya kutafakari mambo ambayo Rais Kenyatta amekuwa akiwashauri wakazi wa Mlima Kenya. Rais Kenyatta amekuwa akionya wakazi wa Mlima Kenya dhidi ya kupigia kura Ruto lakini hawajakuwa makini sasa wamejionea wenyewe,” akasema Bw Kenneth.

  • Tags

You can share this post!

Magharibi, Pwani na Mashariki kuamua mrithi wa Rais Uhuru

Rais wa UAE Khalifa bin Zayed Al Nahyan afariki

T L