• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
Mlima Kenya kuwa na wagombea urais wawili Kabogo akijiondoa

Mlima Kenya kuwa na wagombea urais wawili Kabogo akijiondoa

BENSON MATHEKA na MARY WANGARI

KUJIONDOA kwa aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo kutoka kinyang’anyiro cha urais kumeacha eneo la Mlima Kenya na wagombeaji wawili wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao iwapo wengine hawatajitokeza.

Bw Kabogo ambaye ameunda chama cha Wakenya tujibebe Party, amesema kwamba baada ya kusikiliza maoni ya wengi, atagombea kiti cha ugavana kaunti ya Kiambu kinachoshikiliwa na Gavana James Nyoro.

Kujiondoa kwa Bw Kabogo kumeacha viongozi wawili kutoka eneo la Mlima Kenya – Gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria wa chama cha Usawa Kwa Wote party na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi wa chama cha Democratic Party of Kenya katika kura za urais.

Wa Iria amesisitiza kuwa atakuwa kwenye debe kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya chama chake. Vile vile, Bw Muturi amepuuza madai kwamba yeye ni mradi wa mrengo fulani wa kisiasa akisema eneo la Mlima Kenya lina haki ya kutoa rais baada ya Rais Kenyatta kuondoka mamlakani.

Wagombeaji wakuu wa urais, Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wamekuwa waking’ang’ania kura za eneo la Mlima Kenya.

Bw Kabogo anasema kwamba wagombeaji urais wanaopiga kambi eneo la Mlima Kenya kutafuta kura wataondoka baada ya uchaguzi.

“Tulipoteza mwelekeo tuliporuhusu eneo letu kuvamiwa na wanasiasa. Tunapangwa na ndio sababu tunataka kupigana miongoni mwetu hadi tuungane,” alisema akizungumza na gazeti moja la humu nchini Jumatatu.

Alisema Dkt Ruto alimrai awe mgombea mwenza wake lakini akakataa kwa ajili ya umoja wa jamii za eneo la Mlima Kenya.

You can share this post!

Utangulizi wa uchambuzi wa hadithi ‘Tulipokutana Tena’

Lamu yafaidi miradi mingi ikikamilishwa

T L