• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 3:59 PM
Msimu wa mapanga waandama kampeni

Msimu wa mapanga waandama kampeni

RUTH MBULA na FRED KIBOR

HOFU ya kuzuka kwa ghasia katika uchaguzi imeongezeka nchini baada ya polisi, kwa mara ya pili, kunasa shehena ya mapanga.

Katika Kaunti ya Kisii, polisi wanamzuilia mtu mmoja anayewasaidia katika uchunguzi huku msako mkali ukianzishwa dhidi ya washukiwa wanaopanga kuzua vurugu katika mikutano ya kisiasa.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Kisii, Francis Kooli alithibitisha kuwa mapanga saba yalipatikana yakiwa yamefichwa chooni katika baa moja eneo la Mwembe karibu na mji wa Kisii.

“Tunamzuilia mmiliki wa baa hiyo ili atufafanulie ni jinsi gani na kwa nini mapanga hayo yalikuwa yamefichwa katika baa yake. Tulidokezewa na umma Jumamosi kuhusu mapanga hayo,” alisema Bw Kooli.

Alisema uchunguzi bado unaendelea kuhusu kisa sawa na hicho ambapo mapanga manne yalinaswa karibu na Kisii Sports Club wiki iliyopita.

Kamanda wa Polisi wa Kisii, Francis Kooli ahutubia wanahabari katika kituo cha polisi cha Kisii Central, Juni 12, 2022. Maafisa wa polisi katika kituo hicho walinasa mapanga 12 katika msako unaoendelea wa kuangamiza fujo katika kampeni. PICHA|ONDARI OGEGA

Mapanga hayo yalikuwa miongoni mwa silaha kadhaa zilizopatikana na polisi.Silaha hizo zinazojumuisha pia marungu zilikuwa zinasafirishwa na mwendeshaji bodaboda.

Bw Kooli alisema wanawafuatilia watu wanne wanaoshukiwa kuhusika katika mipango ya kusababisha ghasia.

Alisema mapanga hayo yalikuwa yamefungwa kwenye koti lililoandikwa jina la mgombeaji wa Kisii kwa chama cha UDA na yalikuwa yamefichwa kichakani karibu na Kisii Sports Club ambayo iko mkabala na makao makuu ya Tume ya Uchaguzi (IEBC) katika kaunti hiyo.

“Tumemakinika zaidi kutokana na ripoti za kijasusi tulizopata siku nne zilizopita kuhusu njama za kuzua machafuko na kuvuruga amani katika kaunti hii. Maafisa wetu walidokezewa kuhusu mapanga hayo,” alisema.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu, wanawake wameikosoa Tume ya Kitaifa ya Utangamano (NCIC) kwa kuorodhesha eneo hilo kama kituo kikuu cha ghasia kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti.

Wanawake hao walifanya mkutano wa amani mjini Eldoret Jumamosi wakisema kutaja eneo hilo kama kituo kikuu kuhusiana na ghasia tayari kumesababisha taharuki miongoni mwa wakazi.

Kaunti hiyo inayojumuisha makabila mengi iliathirika zaidi na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/08.

Mnamo Mei 31, NCIC ilisema uwezekano wa ghasia za uchaguzi kuzuka nchini umefikia asilimia 53.43, ikinukuu matokeo ya utafiti uliofanywa kati ya Januari na Aprili ulioshirikisha watu 1,914 kutoka kote nchini.

Tume hiyo iliorodhesha kaunti sita – Nairobi (asilimia 79.85), Nakuru (75.77), Kericho (74.81), Kisumu (72.46), Uasin Gishu (72.25) na Mombasa (71.15) kama maeneo yenye uwezekano mkuu zaidi wa kuzuka kwa ghasia za chaguzi.

Katika ripoti yake, Tume ilisema ilifikia takwimu hizo baada ya kutathmini kwa kina vipengele vitatu; masuala yanayosababisha ghasia (asilimia 53.58) masuala yanayoweza kuzua michafuko (53.4), mifumo dhaifu ya taasisi (53.32).

Utafiti huo uliainisha uwezekano wa kuzuka kwa ghasia katika vitengo vitatu; tishio kuu (kuanzia asilimia 71 kwenda juu), tishio kuu la wastan (asilimia 54-70) tishio la chini la wastan (asilimia 35-53) tishio la chini asilimia (0-34).

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Kauli za viongozi zilenge kuinua maisha ya raia

Nestlé yaongoza mpango wa kukusanya taka za plastiki...

T L