• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Nestlé yaongoza mpango wa kukusanya taka za plastiki katika shule za umma

Nestlé yaongoza mpango wa kukusanya taka za plastiki katika shule za umma

NA SAMMY WAWERU

KAMPUNI ya Nestlé imezindua mpango wa kukusanya taka za plastiki katika shule za msingi za umma, ili kusaidia kudumisha usafi wa mazingira.

Mradi huo unalenga kusafisha mazingira ya shule na viunga vyake, mazingira jirani.

Kwa ushirikiano na Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema), Kenya Extended Producer Responsible Organisation (Kepro) na Wizara ya Elimu, mpango wa majaribio umeanza kutekelezwa katika shule 10 Kaunti ya Nairobi.

Kulingana na Nestlé, mradi huo unalenga kuhamasisha umuhimu wa kukusanya taka na kutunza mazingira, hatua ambayo itasaidia kuangazia athari za tabianchi.

Tabianchi imeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo, kufuatia mabadiliko ya hali ya hewa.

Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Muungano wa Umoja wa Kimataifa (FAO), inaonyesha Kenya ni miongoni mwa nchi zilizolemewa na ukame katika Upembe wa Afrika.

Ukame umekuwa ratiba ya kila mwaka, maeneo jangwa na nusujangwa yakihangaishwa na baa la njaa.

Mradi wa Nestlé kukusanya taka, unatumia bunifu za majaa ya vyuma vyenye umbo la simba.

Ubunifu huo aidha umetajwa kama kivutio kwa wanafunzi, katika oparesheni kusaidia kudumisha usafi wa mazingira.

“Tabianchi ni hali wazi ambayo kila mmoja anahisi athari zake, kufuatia matendo ya binadamu kutolinda mazingira. Ni muhimu tutafakari maamuzi na mienendo yetu, tutathmini vifaa tunavyotumia na sekta ya viwanda ili kulinda mazingira,” akasema Ng’entu Njeru, Mkurugenzi Mkuu Nestlè Kenya wakati wa uzinduzi wa mradi huo jijini Nairobi.

Kwa kushirikisha wanafunzi wakiwa na umri mdogo kulinda mazingira kupitia ukusanyaji taka za plastiki, Bw Njeru alisema mkondo huo utasaidia kuipa afueni sekta kilimo.

Mkurugenzi Mkuu Nestlè Kenya, Bw Ng’entu Njeru na wawakilishi wa wanafunzi kutoka shule 10 za msingi za umma Nairobi, wakati wa uzinduzi wa mradi wa ukusanyaji taka za plastiki, jijini Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Taka za plastiki zimechangia kuharibika kwa udongo – rutuba kudhoofika na uchafuzi wa hewa zinapochomwa.

Akiridhia mpango huo, Mkurugenzi wa Viwango na Masuala ya Ubora katika Wizara ya Elimu jimbo la Nairobi, Bi Salome Wenya alisisitiza haja ya kupalilia wanafunzi wayaenzi mazingira.

Bi Wenya alipongeza kampuni ya Nestlè kwa kuzindua mpango huo, akiutaja kama elimu ya kimsingi itakayosaidia kuboresha mazingira.

“Chini ya Mfumo Mpya wa Masomo, CBC, tunahamasisha kuhusu kilimo kupitia mpango wa 4-K Club,” afisa huyo akaelezea, akiridhia ushirikiano wa serikali na sekta za kibinafsi.

Nema iliahidi kushirikiana na kampuni ya Nestlè kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

“Tutashirikiana kukabiliana na kero ya utuapaji wa taka za plastiki,” akasema Ruth Nderitu, afisa kutoka mamlaka ya mazingira.

Mwaka uliopita, 2021, Rais Uhuru Kenyatta alifufua mradi wa 4-K Club katika shule za umma nchini, mpango unaohusisha wanafunzi kushiriki shughuli za kilimo na ufugaji shuleni.

Nestlé aidha imeahidi kueneza mradi wa ukusanyaji taka shuleni maeneo yote nchini, baada ya kutathmini majaribio yake Nairobi.

Mwaka 2012, kampuni hiyo ya kimataifa ilizindua Nestlé for Healthier Kids program katika kaunti nane Kenya, mpango unaowapa wanafunzi motisha katika shule za msingi za umma kushiriki kilimo.

Mazao, yanalishwa wanafunzi uendelezaji kilimo ukizingatia uzalishaji ulioafikia usawa wa virutubisho vya chakula.

  • Tags

You can share this post!

Msimu wa mapanga waandama kampeni

Sakaja adai ana digrii

T L