• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Msiwape sikio wanaofanya siasa za ukabila, Gavana Mvurya aambia umma

Msiwape sikio wanaofanya siasa za ukabila, Gavana Mvurya aambia umma

Na SIAGO CECE

GAVANA wa Kwale, Bw Salim Mvurya, ameonya umma kuhusu wanasiasa wanaotumia ukabila katika kampeni zao za uchaguzi ujao.

Kulingana na Bw Mvurya, wanasiasa wengi hasa wanaopanga kuwania ugavana wameamua kutumia ukabila wakijaribu kushawishi umma kuwachagua 2022.

Alisema mienendo hiyo ina hatari ya kugawanya wananchi katika kaunti hiyo iliyo na makabila mengi tofauti.

“Kwale ina watu wa makabila yote kutoka kote nchini. Kwa hivyo wale wanaosema eti wanafaa kuchaguliwa kwa sababu wao ni wa kabila fulani, hao wataongoza aje wananchi wote eneo hili?” akasema.

Alikuwa akizungumza mjini Kwale wakati wa hafla ya kufunga rasmi Tamasha la Utamaduni la Kwale.

Jamii tofauti za eneo hilo zilipata nafasi ya kuonyesha utamaduni na talanta zao katika tamasha hilo kupitia kwa muziki na densi.

Kushawishi wapigakura

“Tusiingie katika siasa tukiwa na nia ya kujigawanya kwa misingi ya kikabila,” akasema Bw Mvurya.

Katika kaunti hiyo imekuwa desturi kuwa wagombeaji wengi wa ugavana huchagua wagombea wenza kutoka kwa kabila tofauti na lao.

Kando na hilo, imeibuka kuwa baadhi ya wagombeaji wanatumia kabila la viongozi waliopo kwa sasa kushawishi wapigakura kuchagua kiongozi wa kabila lingine wakati wa uchaguzi wa mwaka 2022.

Idadi kubwa ya wenyeji katika kaunti hiyo huwa ni wa jamii za Wadigo na Waduruma.

Bw Mvurya, ambaye anatumikia kipindi chake cha mwisho cha ugavana humpigia debe naibu wake, Bi Fatuma Achani kurithi kiti hicho.

Aliambia wananchi waliohudhuria tamasha hilo kujiepusha pia na wanasiasa wanaobagua wenzao kwa misingi ya kijinsia.

“Rais wa Tanzania Samia Suluhu amedhihirisha kuwa mwanamke anaweza kuwa kiongozi wa taifa. Kwa hivyo wale wanaosema haiwezekani Bi Achani kuwa gavana wa pili wa kaunti hii ni waongo,” akasema.

Hivi majuzi, Bi Achani ambaye anatarajiwa kuwania nafasi hiyo kupitia kwa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) alitangaza atamchagua Diwani wa Samburu Chengoni, Bw Chirema Kombo, kuwa mgombea mwenzake.

Wawili hao walipokewa katika Chama cha UDA na Naibu Rais William Ruto, wakati alipozuru kaunti hiyo Jumamosi.

Wengine wanaomezea mate kiti hicho ni Bw Lung’anzi Chai, Spika wa Bunge la Kaunti ya Kwale Sammy Ruwa, mfanyabiashara Gereza Dena na aliyekuwa waziri Chirau Ali Mwakwere.

Bw Chai ambaye awali alikuwa akiotea tikiti ya UDA, aliamua kubadili msimamo kuhusu chama atakachotumia huku akidai kunyimwa haki ikionekana Bi Achani atapata tikiti ya moja kwa moja katika chama hicho cha Dkt Ruto.

You can share this post!

Vipusa wa Uingereza waweka rekodi mpya ya ufungaji mabao...

Kipchoge, Chepng’etich roho mkononi tuzo ya...

T L