• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Mudavadi apuuzilia mbali dai la kuwepo juhudi kufufua NASA

Mudavadi apuuzilia mbali dai la kuwepo juhudi kufufua NASA

Na WANDERI KAMAU

KINARA wa ANC, Musalia Mudavadi, amekanusha ripoti kuhusu uwepo wa juhudi mpya kati yake na kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka (Wiper) za kufufua muungano wa NASA.

Alhamisi iliyopita, Bw Odinga aliwarai vinara hao kuungana tena ili kuimarisha uwezekano wa kuibuka washindi katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Odinga alisema ili kuboresha nafasi yao kutwaa ushindi, lazima vigogo hao wanne, akiwemo Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) kurejea pamoja.

Bw Odinga alitoa kauli hiyo Jumatatu wakati wa misa ya wafu ya mbunge wa zamani wa Gem, Jakoyo Midiwo, aliyefariki wiki iliyopita.

Hafla hiyo ilifanyika katika Kanisa la Citam, Valley Road, ambapo Bw Mudavadi na Bw Musyoka walikuwepo.

Bw Odinga alisema ni muhimu kwa viongozi hao kuungana kwa manufaa ya nchi.“Maisha ya Jakoyo yanapaswa kurejesha umoja miongoni mwetu,” akasema Bw Odinga.

Lakini jana, Bw Mudavadi alikanusha madai kuhusu uwepo wa juhudi za kufufua muungano huo, badala yake akizitaja kuwa za “kipuuzi.”

“Hakuna juhudi kama hizo zinazoendelea. Huo ni upotoshaji tu,” akasema Bw Mudavadi jana.

Kauli yake inajiri huku juhudi za ODM kubuni muungano wa kisiasa na Chama cha Jubilee (JP) zikiripotiwa kushika kasi.

Kulingana na wadadisi wa siasa, misimamo mikali ya Mabw Mudavadi na Musyoka inaonyesha kuwa bado hawamwamini Bw Odinga na huenda juhudi za kuwaunganisha vigogo hao zisizae matunda.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akionekana kuwarai vigogo hao kuungana tena, akisema huenda akamuunga mkono mmoja wao kuwa mrithi wake.

Wiki iliyopita, Bw Musyoka alisema kwamba hawezi tena kumuunga mkono Bw Odinga kuwania urais 2022, akieleza kuwa ni zamu ya Raila “kurejesha mkono.”

“Siwezi kumuunga mkono Raila kwa mara ya tatu. Afadhali nirejee kwetu,” akasema Bw Musyoka.Kiongozi huyo alikuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga katika uchaguzi kuu za 2013 na 2017.

Bw Mudavadi amekuwa akisisitiza atakuwa debeni kwenye uchaguzi huo, hali inayozua mkanganyiko kuhusu ikiwa juhudi za kuifufua NASA zitafaulu.

Wadadisi wa siasa wanasema kuwa hali ya kutoaminiana miongoni mwa vigogo hao ndiyo itakayoamua ikiwa mikakati ya kubuni muungano mpya wa kisiasa itafaulu au la.

Tayari, muungano wa One Kenya Alliance (OKA) unaowashirikisha Bw Musyoka, Bw Mudavadi, Bw Wetang’ula na Seneta Gideon Moi (Kanu) unaonekana kuyumba.

Hii ni baada ya Bw Moi kukwepa kuhudhuria mikutano muhimu kuhusu ulainishaji wa mikakati na mipango yake ya kisiasa.

Baadhi ya ripoti zinadai kuwepo juhudi mpya za kuwaunganisha Bw Odinga na Gideon kuwania urais mwaka ujao.

“Misimamo mikali ya Mudavadi na Kalonzo inachangiwa na hali ya kutoaminiana miongoni mwa vigogo hao. Hicho ndicho kibarua kikubwa anachokumbwa nacho Rais Kenyatta katika kurejesha umoja uliokuwepo awali,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Gavana Charity Ngilu (Kitui) amesema atajitolea kuwaunganisha vigogo hao tena.Katika mazishi ya mbunge wa zamani wa Kibwezi, Kalembe Ndile, wiki iliyopita, Bi Ngilu alionya vigogo hao kwamba ikiwa hawataungana, basi wanatoa nafasi kwa Naibu Rais William Ruto kuibuka mshindi.

You can share this post!

Hofu bwanyenye mwingine mashuhuri akiuawa

Wapwani si wavivu, Shahbal asema