• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 11:55 AM
Mudavadi kuteua mgombea mwenza kutoka Mlima Kenya

Mudavadi kuteua mgombea mwenza kutoka Mlima Kenya

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Amani National Congress (ANC) amedokeza kuwa kuna uwekezekano mkubwa kwamba atateua mgombeaji mwenza wake kutoka eneo la Mlima Kenya.

Hata hivyo, alisema atafanya uteuzi huo “wakati mwafaka lakini sio sasa.”

Akiongea Jumanne, Septemba 7, 2021 asubuhi katika kituo cha Inooro FM, Bw Mudavadi alisema alifikia uamuzi huo kwa sababu eneo la Mlima Kenya lina idadi kubwa ya wapigakura na “watu wana ujuzi mkubwa kisiasa”.

“Kuna dalili kuwa eneo la Mlima Kenya halitatoa mgombeaji urais katika uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo, kwa sababu eneo hili limewahi kutoa marais watatu tangu Kenya ilipopata uhuru, ni wengi na wana mchango mkubwa katika uchumi, naona ni bora kuteua mgombeaji mwenza kutoka eneo hilo,” akasema.

“Hata hivyo, nitafanya hivyo wakati ukifika. Kilicho muhimu wakati huu ni kwangu kuuza sera zangu za kiuchumi kwa wakazi wa Mlima Kenya na Wakenya kwa jumla,” Bw Mudavadi akasema.

Aliwasifu wakazi wa Mlima Kenya akiwataja kama wafanyabiashara shupavu na wanaochangia ustawi wa Kenya kwa kiwango kikubwa.

Bw Mudavadi aliwataka wakazi wa eneo hilo kuchunguza kwa makini ahadi wanazopewa na wagombeaji urais kutoka maeneo mengi ili waweze kufanya “maamuzi ya busara siku ya kupiga kura mnamo Agosti 9, 2022.”

Kauli ya Kiongozi huyo wa ANC inaonekana kuashiria kuwa huenda Muungano mpya wa One Kenya Alliance (OKA) hautawasilisha mgombeaji mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye pia ni mmoja wa vinara katika muungano huo pia ameapa kuwania urais “liwe liwalo”. Nyota wengine katika OKA ni kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi.

Vile vile, kauli ya Bw Mudavadi inaashiria wazi kwamba hatakubali shinikizo za Rais Uhuru Kenyatta kwamba yeye na vinara wenzake wa OKA waungane na kiongozi wa ODM Raila Odinga ili watoe mgombeaji mmoja atakayepambana na Naibu Rais William Ruto debeni.

Katika siku za hivi karibuni, Bw Mudavadi amezidisha kampeni zake za kusaka uungwaji mkono katika eneo pana la Mlima Kenya.

Kwa mfano, tangu Juni 2021, kiongozi huyu wa ANC amezuru Kaunti ya Nyeri mara mbili. Vile vile, amezuru Kaunti ya Murang’a.

Isitoshe, Bw Mudavadi ametembelea Nakuru na Kiambu. Mnamo Jumamosi wiki jana mwanasiasa huyo alizuru Kaunti ya Nyandarua ambako aliongoza shughuli ya kuchanga pesa kusaidia kanisa moja la Katoliki eneo hilo.

Duru zinasema kuwa Bw Mudavadi anapania kufanya ziara katika Kaunti ya Meru kusaka uungwaji mkono.

Amebuni mpango wa kiuchumi kwa jina “Uchumi Bora, Pesa Mfukoni” ambao anasema ni jawabu kwa matatizo ya kiuchumi yanayosibu Wakenya wakati huu.

Katika mahojiano yake katika redio ya Inooro FM, Jumanne, Bw Mudavadi aliwataka wakazi wa eneo la Mlima Kenya kuzingatia zaidi sera na ajenda za maendeleo ambazo wagombeaji urais wananadi ili kubaini manufaa yao kwao.

You can share this post!

IEBC yakana ‘kumsaidia’ Ruto

Pigo kwa Spurs baada ya mshambuliaji Son Heung-min kupata...