• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Musalia, Wetang’ula wasita vyama vyao kumezwa na UDA

Musalia, Wetang’ula wasita vyama vyao kumezwa na UDA

NA RICHARD MUNGUTI

VYAMA vya kisiasa katika muungano wa Kenya Kwanza vinasita kuvunjiliwa mbali kuunda chama kimoja cha United Democratic Alliance (UDA).

Ford-Kenya chake Moses Wetang’ula na kile cha Amani National Congress (ANC), vinahofia kutokomea kabisa na kutiwa katika kaburi la sahau endapo vitavunjiliwa mbali na kumezwa na UDA.

Kinyume na uchaguzi mkuu wa 2017 Ford-Kenya na ANC havikushinda viti vingi vya kisiasa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9,2022.

Kumezwa kwa vyama hivi vya kisiasa na UDA kunaambatana na Kifungu nambari 77 (1) cha Katiba kinachosema mawaziri na maafisa wakuu wa umma hawapasi kuwa viongozi wa vyama vya kisiasa.

“Afisa wa umma (wakiwamo mawaziri) haruhusiwi kuwa kiongozi wa chama vya kisiasa,” Kifungu nambari 77 (1,2) cha Katiba kimeweka wazi.

“Kujiuzulu kwa Musalia Mudavadi kama kinara wa ANC kutaua chama hicho kabisa. Ikiwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula atajiuzulu kama kiongozi wa Ford-Kenya vile vile chama hicho kitatokomea kabisa,” asema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Bw Martin Andati.

Pendekezo la Rais William Ruto kuwe na chama kimoja cha kisiasa limezua tumbo joto katika muungano huo wa Kenya Kwanza (KKA).

Muungano wa KKA unataka kuiga mfano wa chama cha Jubilee ambacho kilimeza vyama vidogo vidogo vya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Washauri wa Rais Ruto wanaendelea kupokea uungwaji mkono na vyama  vilivyounga mkono KKA wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Chama cha UDA, kilichounda serikali kinafuata nyayo za Jubilee ijapokuwa hakuna uhakika vyama vilivyounga mkono KKA vitakubaliana na pendekezo hilo.

Tayari Waziri  mteule Moses Kuria ameeleza nia yake ya kukivunja Chama Cha Kazi (CCK) kujiunga na UDA.

Muungano tanzu wa Jubilee ulibuniwa Septemba 2016 ukiwa na vyama 12 vya kisiasa.

Muungano huu ulitwaa ushindi katika kaunti nyingi..

Jubilee klishinda viti 171 katika bunge la kitaifa. Viti vya ubunge vilikuwa 140 kati ya 290, ulishinda wawakilishi wa kike 25 kati ya 47 na pia ulifanikiwa kuwateua wabunge maalum 12.

Chama hicho kilifaulu kupata thuluthi tatu ya viti katika bunge sawa na asili mia 62.

Chama cha Jubilee kilishinda viti vya ugavana 25 kati ya 47 na kilikuwa na seneta 34 kati ya 67.

Ikiwa vyama 15 vya KKA vitakubali kumezwa na UDA basi katika uchaguzi mkuu wa 2027 havitashiriki vikiwa huru katika zoezi hilo.

Vyama vinavyounda KKA ni pamoja na: UDA, Amani National Congress (ANC), Ford Kenya, Chama Cha Kazi (CCK), Communist Party of Kenya (CPK), The Service Party (TSP), Tujibebe Wakenya Party, Farmers Party, Devolution Party of Kenya, Economic Freedom Party, Umoja na Maendeleo Party na Democratic Party.  Vingine ni National Agenda Party of Kenya, Grand Dream Development Party, United Democratic Movement (UDM) chake Seneta Ali Roba na Chama Cha Mashinani chake aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto.

Mwenyekiti wa UDA Bw Johnson Muthama amedokeza kwamba pendekezo lao ni kuwe tu na chama kimoja cha UDA kitakachowadhamini wawaniaji viti katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Muthama alisema kuwa UDA hakitavishurutisha vyama hivyo kuvunjwa katika jitihada za kujiunga na chama hiki kinachotarajiwa kuwa kikubwa na chenye ushawishi mkubwa kisiasa.

“Tunataka kushiriki katika uchaguzi mkuu wa 2027 kama chama kimoja kinachojulikana UDA. Uchaguzi wetu utaegemea UDA na sasa tunaendelea na uchaguzi mashinani. Yeyote anayetaka kujiunga na UDA yuko huru kuvunja chama chake na kujiunga na UDA. Milango iko wazi. Anayetaka aje,” mwenyekiti huyo wa UDA alisema.

Mbunge Didmas Barasa amesema ifikapo 2027 kutakuwa na chama cha UDA kitakachowadhamini wawaniaji viti.

Wale ambao hawataathirika ni Rais Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua.

  • Tags

You can share this post!

Raila anusa mpango wa kando kisiasa

Wakenya kubeba zigo la deni la ujenzi wa SGR

T L