• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mvutano wa Malala, Khalwale hatari kwa Kenya Kwanza

Mvutano wa Malala, Khalwale hatari kwa Kenya Kwanza

NA BENSON AMADALA

UBABE wa kinyang’anyiro cha ugavana katika Kaunti ya Kakamega kati ya Seneta Cleophas Malala na mtangulizi wake, Boni Khalwale, unatishia kuvuruga kampeni za Muungano wa Kenya Kwanza katika eneo hilo.

Seneta Malala, ambaye ni mshirika wa karibu wa kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, anasisitiza wakati umefika kwa kiongozi kijana kuchukua uongozi wa kaunti hiyo.

Bw Malala ambaye pia ndiye mwenyekiti wa ANC katika kaunti hiyo, anakabiliana naDkt Khalwale, ambaye ni mshirika wa karibu wa Naibu Rais William Ruto katika eneo hilo.

Mvutano kati ya viongozi hao wawili unatarajiwa kuathiri kampeni za Kenya Kwanza, hasa unapolenga kupata uungwaji mkono kutoka kwa wenyeji. Eneo hilo limekuwa likipigia kura chama cha ODM.

Uchaguzi mkuu wa Agosti unapokaribia, eneo hilo linaonekana kudhibitiwa na mirengo ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza.

“Niko kwenye kinyang’anyiro cha ugavana katika Kaunti ya Kakamega kwa sababu tunahitaji uongozi utakaoleta mabadiliko katika eneo hili. Ni miongoni mwa viongozi vijana ambao wamejitokeza sana kutetea mfumo wa ugatuzi. Hiyo ndiyo sababu nimejitosa kwenye kinyang’anyiro hicho,” akasema Bw Malala.

Msimamo wa Bw Malala umezua mvutano katika Kenya Kwanza, hali inayotarajiwa kuleta ushindani mkali kati ya wanasiasa hao wawili.

Dkt Khalwale, maaarufu kama ‘Bullfighter’, anawania wadhifa huo kwa mara ya pili.

Ushindani wa kisiasa katika muungano huo unaonekana kuongezwa na kauli ya Bw Malala kwamba lazima nafasi ya mgombea urais itengewe Bw Mudavadi.

Alisema kuwa Bw Mudavadi anapaswa ‘kupewa shukrani’ kwa kujiunga na Dkt Ruto pamoja na Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) kwa kutengewa nafasi ya mgombea-mwenza.

“Dkt Ruto anapaswa kumteua Bw Mudavadi kama mgombea-mwenza wake katika muungano wa Kenya Kwanza. Hili ni suala tunalopaswa kujadiliana na kukubaliana kulihusu. Tuko wazi kwenye majadiliano yetu na tutatarajia kwamba tutasuluhisha suala hilo kwa amani,” akasema Bw Malala kwenye mahojiano Jumatatu.

Shinikizo za Bw Malala zimezua utata katika muungano huo, baada ya mbunge Rigathi Gachagua (Mathira), kusema kwamba suala la mgombea-mwenza lilikuwa tayari lishaamuliwa.

Bw Gachagua, ambaye ni mshirika wa karibu wa Dkt Ruto katika ukanda wa Mlima Kenya, alisema kuwa wakati Mabw Mudavadi na Wetang’ula walijiunga na Dkt Ruto, uamuzi huo ulikuwa ushapitishwa.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi waisifia serikali kwa kumwaga mamilioni kupanua...

Majangili wavamia kituo na kuua afisa, waiba bunduki 4 na...

T L