• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 3:45 PM
Mwaka 2020 ulivyosambaratisha mipango ya Waititu

Mwaka 2020 ulivyosambaratisha mipango ya Waititu

Na SAMMY WAWERU

Ferdinand Ndung’u Waititu si mgeni machoni mwa umma kutokana na umaarufu wake na wa aina yake katika ulingo wa siasa.

Bw Waititu na ambaye kumbukumbu zinaonyesha alizaliwa mnamo Januari 1, 1962, ni mwanasiasa anayejulikana kwa vituko na sarakasi, hususan kutokana na matamshi ya wakati akiwa Gavana wa Kiambu, alipodai “mto unaweza kusongeshwa badala ya majengo ya watu kubomolewa”.

Alitoa matamshi hayo kufuatia ubomozi wa baadhi ya majengo Nairobi uliotekelezwa na serikali kuu kwa ushirikiano na ya kaunti ya Nairobi, yaliyosemekana kuwa katika ardhi zilizonyakuliwa na pia kandokando mwa mito.

Waititu alifanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne 1981, na ambapo alijiunga na Chuo Anuwai cha Kenya (Kenya Polytechnic, kwa sasa Technical University of Kenya).

Baadaye, aliendeleza masomo ya elimu ya juu Punjab, nchini India, na kufuzu kwa Shahada ya Masuala ya Biashara kutoka Sri Guru Singh College of Commerce, mwaka wa 1991.

Alijitosa katika ulingo wa siasa 2002, baada ya kuchaguliwa kama diwani wa wadi ya Njiru, Nairobi. Pia aliwahi kuhudumu kama naibu meya Nairobi.

Kati ya mwaka wa 2008 – 2013, Bw Waititu, almaarufu ‘Baba Yao’ alihudumu kama mbunge wa Embakasi na pia Naibu Waziri wa Maji, chini ya utawala wa serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga ambaye alikuwa Waziri Mkuu.

Katika uchaguzi mkuu wa 2013, aliwania ugavana Nairobi, japo akabwagwa na Dkt Evans Kidero, aliyehudumu hadi 2017.

Licha ya mahakama kuu 2014 kumtaja Waititu kama “kiongozi asiyepaswa kushikilia afisi yoyote ile ya umma kutokana na matamshi ya chuki na uchochezi wa vita” aliyorusha wakati akiwa mbunge Embakasi, 2015 alifanikiwa kuchaguliwa mbunge wa Kabete, Kaunti ya Kiambu kupitia uchaguzi mdogo ulioandaliwa kufuatia kifo cha mbunge wa eneo hilo George Muchai.

Ni katika zoezi la mchujo kwenye mrengo tawala wa Jubilee (JP), Aprili 2017 Waititu aliibuka mshindi na baadaye kumrithi Gavana William Kabogo, katika uchaguzi mkuu Agosti 2017.

Chini ya JP na mgombea mwenza James Nyoro (gavana wa sasa Kiambu), alizoa idadi ya juu ya kura, 740, 986 dhidi ya mpinzani wake Kabogo aliyepata 199, 293, ambaye alitetea kuhifadhi kiti chake kama mgombea wa kujitegemea.

Masaibu yalianza kumuandama alipotajwa kushiriki ufisadi, ufujaji wa mali ya umma na matumizi mabaya ya ofisi Kiambu.

Aidha, alisemekana kujaribu kumnyang’anya mjane mmoja kipande chake cha ardhi Thika, chenye thamani ya mamilioni ya pesa.

Ni madai jumla yaliyochochea madiwani Kiambu Desemba 2019 kupiga kura kumuondoa ofisini, licha ya hatua hiyo kukosolewa kwa msingi yalichochewa kisiasa.

Jumla ya MCA 63 walipitisha mswada wa kumng’atua mamlakani, mmoja pekee akiupinga.

Januari 28, 2020 bunge la seneti liliidhinisha uamuzi wa madiwani Kiambu kumfurusha Bw Waititu, spika Ken Lusaka baadaye akachapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali kung’atuliwa kwake.

Kilichofuata kikawa Naibu wake, James Nyoro kuapishwa rasmi kama Gavana Kiambu.

Waititu, 58, anatajwa kama kiongozi aliye na nyoyo tisa, kutokana na masaibu aliyopitia akiwania viti vya kisiasa ila hafi moyo.

Kufuatia kuondolewa mamlakani kwa Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, Desemba 2020 kwa madai ya kushiriki ufisadi, ufujaji wa mali ya umma na matumizi mabaya ya afisi, harakati za maandalizi ya uchaguzi mdogo zikiendelea, Waititu ametangaza nia yake kumrithi Sonko.

Afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa nchini tayari imemuidhinisha kuwania ugavana Nairobi kama mgombea wa kujitegemea.

Aidha, Waititu amepeleka stakabadhi zake kwa tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC), akisema uamuzi kugombea ugavana Nairobi “unanirejesha nyumbani nilikoanza safari yangu katika ulingo wa kisiasa”.

Hatua hiyo hata hivyo imekosolewa na baadhi ya wapinzani wake kisiasa, tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini (EACC) ikisema kiongozi yeyote aliyetajwa kuhusishwa na kashfa za ufisadi hapaswi kuwania kiti cha kisiasa wala kushikilia afisi ya umma.

You can share this post!

EACC yawazima Sonko na Baba Yao

Watoto mayatima wafadhiliwa kuejerea darasani