• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Najuta sana kutounga Wanyonyi Ugavana Nairobi, Igathe hakutosha – Raila

Najuta sana kutounga Wanyonyi Ugavana Nairobi, Igathe hakutosha – Raila

NA CECIL ODONGO

KINARA wa Upinzani Raila Odinga amejutia hatua ya Muungano wa Azimio kutomkabidhi Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi tiketi ya kuwania Ugavana wa Nairobi kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Bw Odinga alikiri hadharani kuwa alisukumwa kutompa Bw Wanyonyi tiketi akisema kuwa aliyepokezwa tiketi hakuwa maarufu ndiposa Azimio ilikosa kutwaa ugavana.

Katika uchaguzi wa 2022, bendera ya Azimio kwenye ugavana ilipeperushwa na mwanauchumi Polycarp Igathe (Jubilee) huku mgombeaji mwenza wake akiwa Philip Kaloki (Wiper).

“Mimi mwenyewe najuta kwa sababu mimi ndio niliambiwa niambie Tim awache na akawa muungwana akakubali. Tulimpa mgombeaji mwenza akasema anarudi Westlands. Hatukushindwa Ugavana kutokana na kutokuwa na watu ila mwaniaji ambaye tulikuwa naye, ndiye hakuwa sawa,” akasema Bw Odinga.

“Kama tulishinda Urais, Useneta na Mbunge Mwakilishi wa Kike, tunashindwa aje ugavana? Hatungeshindwa Ugavana iwapo tungekuwa na mwaniaji aliyependwa na raia. Kati ya viti 17, vitatu peke yake ndivyo viliekekea upande wa Kenya Kwisha (Kenya Kwanza),” akaongeza Bw Odinga.

Alikuwa akihutubu kwenye eneobunge la Westlands Nairobi wakati alipokutana na viongozi wa makanisa kutoka Magharibi mwa Kenya. Mkutano huo pia uliohudhuriwa na viongozi wa upinzani akiwemo aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, Seneta Edwin Sifuna na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nairobi Esther Passaris.

“Aliyeokoka hahubiriwi injili, mimi mnakuja kununiambia mambo ya Tim?  Hapana,” akasema Bw Odinga huku akishangaliwa na vijana.

Kinara huyo wa upinzani alimminia sifa Bw Wanyonyi ambaye ni nduguye Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula. Aliahidi kusimama naye hadi 2027 kwenye azma yake ya kuwania Ugavana akimwaahidi kuwa mara hii, atamshika mkono kama ‘kijana’ wake.

“Mimi najua mambo ya Tim, nasema tuangalie mbele na vijana wetu ambao wamehitimu umri wa miaka 18 wachukue kura. Tunataka kuzidisha idadi ya watu wetu ambao wanachukua kura na hiyo itakuja tu iwapo watachukua kitambulisho bure,” akasema.

Waziri huyo mkuu wa zamani alishutumu utawala wa Rais Ruto kuhusu kuwataka watu walipie kitambulisho, akiahidi kuwa kamwe hataruhusu hilo nchini.

“Tim tumetoka naye mbali, amesoma vizuri anajua kazi yake, anaelewa mambo ya uchumi. Mtu kama huyu nataka apewe fursa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Seneta maalum ajiunga na wachuuzi wanaoishi na ulemavu...

Pasta atoa ushuhuda jinsi alivyoepuka kupata virusi vya...

T L