• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Ngilu atoa hakikisho kortini kuwa atalipa madaktari mishahara ya miezi minne

Ngilu atoa hakikisho kortini kuwa atalipa madaktari mishahara ya miezi minne

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA CHARITY Ngilu jana aliambia mahakama kuu kwamba atalipa madaktari 20 mishahara ya miezi minne iliyokuwa haijalipwa.

Bi Ngilu alitoa hakikisho hilo mbele ya Jaji Monicah Mbaru alipofika mbele yake kueleza sababu za kuchelewesha mishahara ya madaktari 20 kwa muda wa miezi minne.Gavana huyo aliomba mahakama apewe siku 30 kuwalipa madaktari mishahara wanayodai ya miezi minne.

Mnamo Novemba 5 2021, Jaji Mbaru alimwagiza Bi Ngilu afike kortini akiwa ameandamana na Afisa Mkuu anayesimamia masuala ya afya katika serikali ya Kaunti ya Kitui na pia katibu mkuu katika gatuzi hilo.

Bi Ngilu, waziri wa afya Bw Kitetu na katibu mkuu kaunti hiyo Bw Japhet Muthengi walifika mbele ya Jaji Mbaru kueleza sababu za kukaidi agizo hilo la mahakama wawalipe madaktari hao mishahara ya miezi minne.“Nitawalipa madaktari hao katika muda wa siku 30,” Bi Ngilu alimweleza Jaji Mbaru.

Pia Bi Ngilu aliwarai madaktari zaidi ya 40 waliotoroka kaunti ya Kitui kwenda kufanyakazi kwengineko warudi kuendelea na kazi kwa vile suala la uhaba wa pesa limesuluhishwa.

Bi Ngilu aliiomba mahakama iruhusu walalamishi na maafisa wakuu katika kaunti ya Kitui kufanya mashauri kulainisha masuala tata yote kisha kesi itajwe Desemba 10,2021, ithibitishwe ikiwa madaktari walipokea mishahara yao na masuala mengine waliyolalamikia yamesuluhishwa.

Chama cha madaktari nchini KMPDU kilimshtaki Bi Ngilu na serikali ya kaunti ya Kitui kwa kutowalipa madaktari mishahara ya miezi minne kinyume cha sheria.Madaktari hao walieleza mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi kuanzia Julai 2021.

KMPDU kilidai baadhi ya madaktari walikuwa wametimuliwa kazini kwa madai hawakuwa wakihudumu katika hospitali za kaunti hiyo ilhali walikuwa wameruhusiwa kujiunga na vyuo vikuu Amerika, Scotland na Australia.

You can share this post!

‘Vifaranga’ wa Joho sasa kujitetea kivyao

Kananu kurithi kiti dhaifu cha ugavana jijini

T L