• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Ngoma yaanza

Ngoma yaanza

NA BENSON MATHEKA

KIVUMBI kinatarajiwa kuanza katika Mahakama ya Juu kwa siku kumi na nne zijazo mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga atakapowasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Rais Mteule William Ruto kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Pande zote mbili pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na hasa mwenyekiti wake Bw Wafula Chebukati, zinatarajiwa kuwateua mawakili shupavu kuziwakilisha.

Jana Jumapili, Bw Odinga alisisitiza kuwa atafika kortini leo kuwasilisha kesi kupinga ushindi wa Dkt Ruto.

“Hatuna shaka kwamba watu wa Kenya walizungumza kwa sauti kubwa kupitia kura zao Agosti 9. Sauti zao hazitazimwa na hawatapokonywa ushindi wao,” Bw Odinga alisema akiwa katika kanisa la Jesus Teaching Ministry (JTM), Donholm, Nairobi ambapo aliandamana na mgombea mwenza wake Martha Karua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Duru zinasema kuwa Bw Odinga na Azimio la Umoja One Kenya na Dkt Ruto na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) wameteua mawakili shupavu kuwawakilisha mbele ya majaji saba wa Mahakama ya Juu.

Tayari, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Amos Wako amethibitisha kuwa atawakilisha Azimio kwenye kesi hiyo ambayo Gavana mteule wa Siaya James Orengo, mwenzake wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr, seneta wa kaunti hiyo Dan Maanzo na mbunge wa Rarieda Otiende Omollo watatea Bw Odinga.

Mawakili wengine upande wa Azimio ni Phiroze Norwojee, Profesa Tom Ojienda, Paul Mwangi na Philip Mugor.

Bi Karua na Bw Musyoka ambao pia ni mawakili wanasema kwamba wana hakika ukweli kuhusu dosari katika uchaguzi zitajulikana.

“Tutajua ukweli na utatuweka huru sisi sote kwa kuwa bila haki hatuwezi kuwa na amani ya kudumu,” alisema Bi Karua.

Mawakili wa Azimio watatumia mgawanyiko wa makamishna wa IEBC miongoni mwa ushahidi mwingine kuomba mahakama kufuta matokeo yaliyotangazwa na Chebukati kuonyesha kuwa Dkt Ruto alishinda kura ya urais.

“Wakenya watashangazwa na ushahidi tulio nao. Uchaguzi wa urais ulivurugwa kabisa kupendelea upande mmoja na tutathibitisha hayo,” alisema mmoja wa mawakili wa Azimio ambaye aliomba tusimtaje jina kwa wakati huu.

Upande wa Dkt Ruto unatarajiwa kuongozwa na mawakili Ahmednassir Abdullahi, Elias Mutuma, Nelson Havi, Fred Ngatia, Adrian Kamotho, Collins Kiprono na Emmanuel Kibet miongoni mwa wengine.

Mawakili hao wamekuwa wakisuta Azimio kwa kuwasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Dkt Ruto wakisema wako tayari kuwabwaga mahakamani.

Mawakili wa Chebukati watalazimika kuthibitishia majaji kwamba hakukosea kumtangaza Dkt Ruto mshindi wa uchaguzi wa urais kabla ya kupakia Fomu 34B kutoka maeneobunge 28 kwenye tovuti ya IEBC.

Aidha, mawakili wa Bw Chebukati wanaotarajiwa kuongozwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Profesa Githu Muigai watalazimika kushawishi mahakama kwamba kujitenga kwa makamishna wanne wa IEBC hakukuathiri matokeo ya kura ya urais.

Makamishna hao naibu mwenyekiti Juliana Cherera, Francis Wanderi, Justus Nyang’aya na Irene Masit wanatarajiwa kuwasilisha hati za kiapo kuunga kesi ya Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Wanga kuapishwa wafanyakazi wa kaunti wakigoma

Korti yasitisha ufukuaji mwili wa mfanyabiashara

T L