• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Ngome 4 zawanyima usingizi

Ngome 4 zawanyima usingizi

Na BENSON MATHEKA

WAGOMBEAJI WAKUU wa urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, wamewekeza nguvu wakisaka mbinu za kuwarai wapigakura katika maeneo manne ya Ukambani, Magharibi, Mlima Kenya na Pwani.

Wadadisi wanasema kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga, atakayeshawishi wapigakura wengi katika maeneo hayo kumuunga mkono atakuwa na nafasi nzuri ya kuingia ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Wawili hao wamekuwa wakitumia kila mbinu kutafuta uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya, ngome ya Rais Uhuru Kenyatta ambayo imegawanyika kati ya mashariki na magharibi.

Dkt Ruto ambaye wiki hii amekuwa Mlima Kenya mashariki alikuwa amepenya eneo hilo kabla ya Bw Odinga kuanza kampeni kali akionekana kuungwa mkono na Rais Kenyatta na viongozi wa Jubilee wanaounga handisheki wakiwemo mawaziri, magavana na wabunge kadhaa.

Kulingana na mdadisi wa siasa Simon King’ara, kufikia sasa hakuna mgombea urais anayeweza kudai kwamba ameshawishi Mlima Kenya kumuunga mkono.

“Kura za eneo hilo kwa sasa ziko wazi na itabidi Dkt Ruto na Bw Odinga watie bidii zaidi kuonyesha wakazi kwa nini wanafaa kuwapa kura zao. Kampeni zao eneo hilo zimekuwa mazoezi tu,” asema.

Aidha, wachanganuzi wa siasa wanasema iwapo Dkt Ruto atataka kuwa salama kuhusu kura zake za urais, atahitajika kuzoa asilimia kubwa, ya angaa 85 ya kura zitakazopigwa.

Hata hivyo, huenda hilo lisiwe rahisi kutokana na jinsi maeneo kadhaa ya ukanda huo yanavyojiweka tayari kumuunga Bw Raila.

Chini ya Gavana Kiraitu Murungi na Waziri Peter Munya, Bw Odinga yuko katika nafasi ya kuvuna kura kuliko ilivyotarajiwa katika jamii ya Ameru.

Eneo la Magharibi ambalo kwa miaka mingi limekuwa ngome ya Bw Odinga kwa sasa limekuwa telezi kufuatia msimamo mkali wa kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi ambaye anasisitiza atakuwa kwenye debe.

Kulingana na wadadisi wa siasa, Mudavadi akigombea atakuwa tisho kwa Bw Odinga.

“Mudavadi hawezi kukosa kiasi kikubwa cha kura eneo la Magharibi na hii itakuwa tishio kwa Bw Odinga ambaye amekuwa akipata kura kwa wingi eneo hilo,” asema mchanganuzi wa siasa Charles Wekesa.

Anasema kuungana kwa Bw Mudavadi na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula kunaweza kumnyima Bw Odinga kura za kaunti za Bungoma na Trans Nzoia.

“Dkt Ruto pia amepenya sehemu za eneo hilo kupitia washirika wake na hii inampa Bw Odinga tumbojoto,” asema.

Bw Odinga, Jumamosi alianza ziara yake katika Kaunti ya Trans Nzoia kuvumisha kampeni yake ya Azimio la Umoja.

Wachanganuzi wanasema Bw Odinga lazima afanye juu chini asipoteze kura za eneo la Ukambani, ngome ya kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka ambaye alikuwa mgombea mwenza wake 2017.

Ingawa Bw Odinga amewavuta magavana watatu wa kaunti za Ukambani, Bw Wekesa anasema kwamba itakuwa vigumu kupata zaidi ya kura milioni 1.8 za eneo hilo bila kushirikiana na Bw Musyoka.

“Ushawishi wa Bw Musyoka hauwezi kulinganishwa na usuhuba wa kisiasa wa Bw Odinga na Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni),” asema.

Katika eneo la Pwani ambalo kwa miaka mingi pia limekuwa ngome ya Bw Odinga, Dkt Ruto ameonekana kupenya kwa kishindo, hatua inayoweza kuvuruga hesabu ya waziri huyo mkuu wa zamani.

Mbali na Dkt Ruto kujishindia wanasiasa kadhaa wa ODM, kuna juhudi za kuunganisha vyama vyenye mizizi eneo la Pwani.

Tayari Gavana wa Kilifi, Amason Kingi anapepea na chama chake cha PAA.

“Hili ni eneo ambalo limekamua pumzi nyingi na pesa za Dkt Ruto akijaribu kufifisha umaarufu wa Bw Odinga,” asema Bw Wekesa.

Washirika wa miaka mingi wa Bw Odinga eneo la Pwani, akiwemo Kingi na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho wameonekana kutomchangamkia katika siku za hivi majuzi.

You can share this post!

3 walazwa hospitalini Marsabit baada ya kushambuliwa

Wanafunzi 302 ndani kwa uchomaji shule

T L