• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Niliogopa umwagikaji wa damu 2017 – Uhuru

Niliogopa umwagikaji wa damu 2017 – Uhuru

NA LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta amekiri kuwa alikuwa tayari kujiondoa katika kinyang’anyiro cha urais baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wake wa Agosti 9, 2017.

Rais Kenyatta alisema alikuwa tayari kuchukua hatua hiyo kuzuia umwagikaji wa damu ambao ungesababishwa na machafuko ya baada ya uchaguzi.Kiongozi wa nchi alifungua roho alipokuwa akihutubia mamia ya viongozi wa kidini kutoka eneo la Mlima Kenya katika Ikulu ya Nairobi.

“Mengi yamesemwa kunihusu. Baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa nilitaka kurudi Gatundu baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wangu.

“Ninathibitisha kwamba madai hayo ni ya kweli. Nilitaka kwenda nyumbani. Ikiwa kujiondoa kwangu kungeleta amani nchini, basi nilikuwa tayari kuondoka. Maisha ya binadamu ni muhimu kuliko wadhifa wa urais,” akasema Rais Kenyatta.

Naibu wa Rais William Ruto aliwahi kuambia wazee wa Mlima Kenya katika kikao cha faragha kilichofanyika nyumbani kwake mtaani Karen, Nairobi, kuwa nusura ampige kofi Rais Kenyatta alipoonyesha dalili ya kutaka kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mara baada ya ushindi wake kubatilishwa na Mahakama ya Juu.

Sauti iliyorekodiwa kisiri kutoka kwenye mkutano huo, Dkt Ruto anasikika akisema kuwa alilazimisha Rais Kenyatta kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26, 2017.

“Nilikuwa nimeonya Rais kwamba kulikuwa na ukora mahakamani lakini yeye akasisitiza kwamba mambo yalikuwa shwari. Lakini Mahakama ya Juu ilipobatilisha matokeo ya urais, nilikimbia mara moja Ikulu. Nilipofika Rais aliniambia kuwa alikuwa tayari kujiondoa na kwenda nyumbani Ichaweri (Gatundu, Kaunti ya Kiambu). Kama isingekuwa heshima ningempiga kofi,” akasema Dkt Ruto kwenye mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na mjomba wa Rais Kenyatta, Kung’u Muigai.

Wanasiasa wa muungano wa Azimio wamekuwa wakitumia ufichuzi huo kumponda Dkt Ruto katika kampeni zao huku wakijaribu kumfanya Naibu wa Rais kuonekana kama kiongozi mwenye uchu wa madaraka.

“Ikiwa Ruto alitaka kumpiga kofi Rais Kenyatta, wewe mnyonge atakufanyia nini, si atakukanyaga,” Gavana wa Mombasa aliambia wakazi wa Gatundu wakati wa kampeni wa Azimio.

Alhamisi, Dkt Ruto alijitetea kuwa hakuwa na nia ya kumpiga kofi Rais Kenyatta kama inavyodaiwa.

“Nilisema maneno kuonyesha wazee kutoka Mlima Kenya kuwa Rais Kenyatta ni rafiki yangu wa kweli. Rafiki yako anapokaribia kulemewa inafaa uwe hapo kumsaidia na kumhimiza. Baadhi ya Wakenya wameniunga mkono na wamenukuu kitabu cha Zaburi 27:6 kinachosema kuwa ‘kofi ya rafiki ni bora kuliko busu la rafiki’,” Dkt Ruto aliambia runinga moja ya humu nchini.

Rais Kenyatta jana Ijumaa alisema kuwa angeruhusu Dkt Ruto shavu jingine apige iwapo angethubutu kumzaba kofi.

Alionekana kumshambulia Dkt Ruto kwa ‘kupotosha’ Wakenya kuwa “nilitaka kuachana na urais ilhali wao ndio wamekuwa wakidai kuwa nililenga kubadilisha Katiba kupitia mswada wa BBI ili kusalia mamlakani”.

Rais aliwataka viongozi wa kidini kutoka eneo la Mlima Kenya kutohadaiwa na propaganda za baadhi ya wanasiasa huku Uchaguzi Mkuu ukikaribia.

“Mimi huwa napenda kusema ukweli. Watu wetu wamehadaiwa na wanasiasa fulani kupitia makanisani. Lakini nimefurahi kwani baadhi yenu wamekataa kudanganywa. Kuna waasi wanazurura kote nchini wakisema wamekosewa. Mkataba ni kati ya watu wawili. Ikiwa nimekosea, hata yeye amekosea. Huna haki ya kutafuta uongozi kwa kudanganya, matusi na wizi,” akasema.

Rais Kenyatta alionekana kumpokeza kijiti mwaniaji mwenza wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya Martha Karua huku akisema kuwa atashughulikia masilahi yao.

“Licha ya ukweli kwamba hatujawahi kuwa upande mmoja wa kisiasa na Martha, yeye ni mwadilifu na mwenye kufuata sheria. Ni bora nimfuate mtu aliye na msimamo imara ambaye ni mwadilifu, mkweli na aliye na azma ya kutumikia watu lakini sio yeye binafsi,” alisema.

Rais Kenyatta alisema kuwa anatamani kumaliza muhula wake haraka mwezi Agosti huku akisema kuwa urais ni ‘kazi ngumu’.

“Sitaki kusalia madarakani kama wanavyodai. Hii ni kazi ngumu, hakuna kulala… nyumba hii (Ikulu) imejaa changamoto na miaka kumi kwangu inanitosha. Nangojea Agosti 9 kwa hamu na ghamu niondoke,” Rais alisema.

  • Tags

You can share this post!

Wito serikali ihamasishe jamii kuhusu athari hasi za ngono...

CHARLES WASONGA: Serikali ijayo ifutilie mbali mpango fiche...

T L