• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
‘Nipe nikupe’ ya Ruto na Raila yaendelea

‘Nipe nikupe’ ya Ruto na Raila yaendelea

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amejibu kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga aliyedai kuwa “utawala” wake ni haramu huku akiitisha uchunguzi wa kile alichodai kuwa ni ulaghai uliotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Akiongea Jumatatu akiwa katika eneo la Gatundu alipohudhuria mazishi ya dadake Waziri wa Biashara Moses Kuria – Pauline – Rais Ruto alitaja matakwa ya Odinga kama njama ya kumtisha ili abuni muungano naye.

“Tunajua mahala anakoelekea. Anazua hizi sarakasi zote ili turidhiane naye kisiasa kwa sababu hiki ndicho amefanya kwa marais waliopita tangu Moi,” Ruto akasema.

“Nawaomba mbadilishe, mbinu. Hamtanidanganya. Msahau kuhusu masuala ya handisheki,” Ruto akasema.

Rais alitaja madai ya Bw Odinga kwamba serikali yake sio halali kama madai yasiyo na msingi wowote.

“Tafuta mtu mwingine wa kutisha. Nilichaguliwa na Wakenya mchana peupe na ulipoteza ilhali ulikuwa ukiungwa mkono na wakuu serikalini almaarufu ‘deep State’ upande wenu,” Dkt Ruto akasema.

Rais alisema hatafanikisha masilahi ya watu wachache badala ya masilahi ya Wakenya wengi.

Akiongea katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Bw Odinga pia alirejea ufichuzi wa hivi majuzi uliotolewa na mtu fulani aliyedai kuwa mfanyakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mtu huyo alitoa taarifa ambazo alidai zilionyesha kuwa ni Bw Odinga aliyeshinda katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Ni kwa misingi ya ufichuzi huo ambapo ninasimama hapa leo kutangaza kuwa hatutambui utawala wa Ruto na maafisa wote alioteua,” Bw Odinga akaambia umati wa wafuasi wake waliohudhuria mkutano huo wa Kamukunji, Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

DKT FLO: Nini husababisha kinyesi kuchanganyika na damu?

Haaland afunga hat-trick ya nne katika mechi 19 za EPL na...

T L