• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 7:55 AM
Orengo hatatemwa, Raila afafanua

Orengo hatatemwa, Raila afafanua

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amepuuzilia mbali uvumi unaoenea kwamba chama hicho kinanuia kumvua Seneta wa Siaya James Orengo wadhifa wake wa Kiongozi wa Wachache katika Seneti.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumatano jioni na msemaji wake Dennis Onyango, kiongozi wa ODM alisema chama hicho hakina mpango wowote wa kubadilisha uongozi wa upande wa wachache katika Seneti.

“Kufuatia mabadiliko yaliyofanywa katika uwakilishi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Haki na Masuala ya Sheria, kumekuwa na uvumi usio na mashiko kwamba chama kinaelekea kutekeleza mabadiliko kama hayo katika uongozi wa upande wa wachache katika Seneti,” akasema Bw Onyango.

“Tungependa kufafanua kwamba Mheshimiwa Raila Odinga, kiongozi wa ODM na chama hicho, hana na hakuna mipango ya kumpokonya Seneta James Orengo wadhifa wa Kiongozi wa Wachache,” akaongeza.

Ufafanuzi huo umejiri siku moja baada ya ODM kumwondoa Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo kutoka nafasi yake kama mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) na ambako alihudumu kama Naibu Mwenyekiti.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi Jumatano asubuhi aliambia idhaa ya Dholuo ya Ramogi FM kwamba Bw Amollo alichukuliwa hatua hiyo baada ya kukaidi agizo la kutakiwa kufika mbele ya Bw Odinga kujibu madai ya kukosea ODM heshima.

Kulingana na Bw Mbadi, badala ya Mbunge huyo wa Rarieda kuheshimu agizo hilo, alitisha “kujiuzulu sio tu kutoka kwa kamati ya JLAC bali hata wadhifa wake kama mbunge.”

Hata hivyo, inaaminika kuwa Bw Amollo alipigwa kalamu kwa kuonekana kupinga msimamo wa ODM kwamba mswada wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) upitishwe jinsi ulivyo.

Badala yake mbunge huyo alisemekana kuunga mkono wazo kwamba kufanywe marekebisho kwa ripoti hiyo ili kuondoa kipengele cha pili kinachogawanya maeneobunge 70 mapya miongoni mwa kaunti 28. Kulingana na Bw Amollo, wazo ambalo pia linashikiliwa na Seneta Orengo, wajibu huo ni wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kulingana na kipengele cha 89 cha Katiba.

Hii ndio maana baada ya kutimuliwa kwa Bw Amollo, uvumi umeshamiri kwamba Bw Orengo pia angepigwa kumbo kwa kile kinachodaiwa ni kuhujumu mchakato wa marekebisho ya Katibu kinyume na mapenzi ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

Ni Chelsea na Manchester City kwenye fainali ya UEFA Mei 29

Rais Kenyatta aonya mawaziri wazembe