• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Raila abuni mbinu mpya kujiimarisha

Raila abuni mbinu mpya kujiimarisha

BENSON MATHEKA Na MOSES NYAMORI

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga amezindua mikakati mipya katika juhudi za kuhakikisha anatamba katika siasa, baada ya kushindwa katika jaribio lake la tano la kuingia ikulu.

Akielewa kwamba nafasi yake kuwa rais wa Kenya inazidi kuwa finyu, Bw Odinga ameacha mbinu za awali alizotumia kutoa jasho serikali kupitia maandamano.

Mikakati hiyo ilijitokeza wiki hii alipolaumu jamii ya kimataifa kwa kutoanika anachodai ni dosari zilizomnyima fursa ya kuingia ikulu.

“Walijua kilichokuwa kikifanyika (kuhusu wizi wa kura) lakini hawakufanya chochote kwa sababu hawakufurahishwa na ajenda yetu ya biashara,” Bw Odinga alisema ikiwa ni mara yake ya kwanza kushambulia jamii ya kimataifa kwa msimamo wake kuhusu uchaguzi nchini.

Bw Odinga anasisitiza kuwa, japo hataitisha maandamano anayodai yanaweza kufungua milango ya kesi katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu uhalifu (ICC), atashinikiza mageuzi katika Mahakama ya Upeo anayoshikilia kwamba, ilihujumu ndoto yake ya kuwa rais wa tano wa Kenya.

“Tutapigania mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, mageuzi ya uchumi na idara ya mahakama kuhakikisha kila Mkenya anapata haki,” Bw Odinga alisema Jumatano alipohudhuria uzinduzi wa kitabu cha Mkurugenzi wa chama cha ODM, Odour Ongw’en. Ili kutimiza hayo, Bw Odinga anapanga mikakati ya ndani na nje ya Bunge.

Mpango wake unahusisha kufichua utepetevu na makosa ya serikali kwa ulimwengu huku akimvumisha kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kama sura ya Azimio la Umoja One Kenya.

Hivi majuzi, Musyoka amekuwa msitari wa mbele kutoa taarifa akikosoa serikali ya Kenya Kwanza hasa kuhusu bei za juu za mafuta, mfumko na mipango ya kutimua makamishna wanne wa tume ya uchaguzi wanaochukuliwa kuwa waasi.

Taifa Jumapili imebaini kwamba, Azimio imeweka makataa ya 2024 ya kutekeleza mageuzi katika Mahakama na IEBC.

Bw Odinga alibuni mikakati hii katika mkutano wa faragha wa viongozi wakuu wa Azimio uliofanyika Mombasa mwishoni mwa wiki jana.

Duru zinasema kwamba, waliohudhuria mkutano huo ulioitishwa na Bw Odinga ni Musyoka, Bi Martha Karua, Katibu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Kiongozi wa wachache katika Bunge la Taifa Opiyo Wandayi, naibu wake Robert Mbui, Kiranja wa wachache Junet Mohammed na naibu wake Sabina Chege.

Bw Wandayi atakuwa akitumia sheria za Bunge 44 (2) kukosoa serikali kila Alhamisi na kuzua masuala yenye umuhimu wa kitaifa yanayoathiri nchi.

Sheria ya Bunge 44 (2) inasema kwamba “ kiongozi wa wachache, mwenyekiti wa kamati anaweza kutoa taariifa kuhusiana na majukumu yao ndani ya bunge au shughuli za kamati.”

“Tuko na kazi ya kufanya. Na tuna chaguo gani? Moja sio kusalimu amri. Kusalimu amri sio msamiati katika mageuzi yetu. Tuko na jukumu kama watu kutia nguvu ufanisi wetu na kusimama imara,” Bw Odinga alisema wakati wa hafla ya kuzindua kitabu cha Bw Ong’wen.

Aliongeza; “Vijana wetu wengi hawajui kilichofanyika katika nchi yetu. Wanajiita mahasla kwa sababu hawajui. Tuko tulipo kwa sababu watu waliteseka na baadhi wakafariki kwa ajili ya demokrasia. Na kama haitalindwa basi tunaweza kurudi tulikotoka.”

  • Tags

You can share this post!

IPOA yasifu utendakazi wa polisi wakati wa uchaguzi

KK, Azimio kupambana katika uchujaji wa mawaziri

T L