• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Raila adai Ruto alichangia kufeli kwa Jubilee

Raila adai Ruto alichangia kufeli kwa Jubilee

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amemlaumu Naibu Rais William Ruto kutokana na kufeli kwa serikali ya Jubilee katika kutimiza baadhi ya ahadi ilizotoa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017.

Akiongea mjini Thika, Jumamosi, Januari 15, 2022, katika mkutano wa Azimio la Umoja, Bw Odinga alimlaumu Dkt Ruto kwa kile alichotaja kwamba ni kufeli kutimiza ahadi aliyotoa kabla ya chaguzi za 2013 na 2017.

“Ni mweledi katika kutoa ahadi. Aliahidi viwanja vya michezo katika kila kaunti. Aliahidi wanafunzi wa shule za msingi vipakatalishi lakini sasa anaonekana kuwa ‘analogue’ kwa kuahidi vijana wilbaro,” Bw Odinga akasema katika uwanja wa Thika Green Stadium, kaunti ya Kiambu.

“Amekuwa serikalini kwa miaka minane lakini amefeli kuonyesha Wakenya maendeleo ambayo alileta. Aondoke serikalini nimwonyeshe namna ya kuendesha serikali,” akaongeza.

Bw Odinga alimtaka Dkt Ruto kukoma kulaumu handisheki kati yake (Raila) na Rais Uhuru Kenyatta kama sababu iliyochangia yeye (Ruto) kufeli kutimiza ahadi zake kwa Wakenya.

“Uhuru ametekeleza miradi mingi ya maendeleo baada ya handisheki. Mfano ni mradi wa barabara unaondelea hapa ambao ninaahidi kukamilisha baada ya Uhuru kuondoka mamlakani,” Bw Odinga akasema.

Waziri huyo mkuu wa zamani alitetea ahadi yake ya kutoa Sh6,000 kwa kila familia masikini akisema akisema hiyo sio zawadi au marupurupu anavyodai Dkt Ruto.

“Huu ni mpango wa kuwafaa wasiobahatika katika jamii; wale wanaoishi mijini na wale wanaoishi mashambani,” akaeleza Bw Odinga.

Mikopo nafuu

Bw Odinga alikariri kwamba serikali yake itatilia mkazo suala la kutoa mikopo isiyotozwa riba kwa vijana ili kuwawezesha kunawiri kibiashara.

“Vijana hawahitaji wilbaro wanahitaji ajira na ufadhili wa kuanzisha biashara,” akasema.

Bw Odinga pia alimsuta Naibu Rais kwa ‘kumweka mateka’ Rais Kenyatta katika muhula wake wa kwanza.

“Uhuru aliwekwa mateka na watu waliotaka afeli kisha wajitenge na kufeli huko ili warejee na ahadi nyingine za uwongo,” Bw Odinga akasema huku akiongeza kuwa ni baada ya handisheki ambapo Rais Kenyatta alianza kufanya kazi “sawasawa”.

Lakini akiendesha kampeni zake katika kaunti ya Nairobi, Alhamisi na Ijumaa, Dkt Ruto alimlaumu Bw Odinga kwa kuchangia kushindwa kwa Jubilee kutimiza ahadi ilizotoa kwa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017.

“Hii ndio maana naahidi hapa leo (Ijumaa) kwamba nitakamilisha mpango wa maendeleo chini ya mwavuli wa Nguzo Nne za Maendeleo (Big Four Agenda) baada ya Rais Kenyatta kustaafu. Hii ni kwamba mpango huo ulivurugwa na yule jamaa wa kitendawili alipoingia katika serikali na kulete reggae na ajenda ya kubadilisha katiba kugawa viti kwa viongozi wachache,” akasema Dkt Ruto katika eneobunge la Roysambu.

You can share this post!

Lempurkel ashtakiwa upya kwa matamshi ya uchochezi

Bayern na Lewandowski waweka rekodi mpya za ufungaji wa...

T L