• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Raila akubali mfupa wa Ruto

Raila akubali mfupa wa Ruto

NA SAMWEL OWINO

KIONGOZI wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, ametishia kukataa mswada unaolenga kuanzisha Afisi ya Kiongozi wa Upinzani iwapo hautalazimisha mwelekeo wa jinsi serikali inavyopaswa kukosolewa na kupigwa msasa.

Kupitia msemaji wake Denis Onyango, Bw Odinga aliambia Taifa Jumapili kwamba anasubiri kuona yaliyomo kwenye mswada huo kabla ya kuuzungumzia lakini akaonya iwapo utaenda kinyume cha katiba, basi hataukubali.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu pendekezo la kubadilisha katiba ili kuunda afisi ya kiongozi wa upinzani, Bw Odinga alisema anasubiri kuona yaliyomo kwenye pendekezo hilo.

“Tunasubiri kuona mswada huo wakati wowote na popote utakapotoka ili tuushughulikie utakavyokuwa. Hata hivyo, hatutarajii mswada unaoeleza wakati, wapi na jinsi serikali inapaswa kupingwa na ni nani anayefaa kufanya hivyo,” Bw Odinga alisema.

“Hali kama hiyo itakuwa ya kwanza kuwahi kutokea. Tutaichukulia kama tishio jipya kwa katiba na tutaushughulikia kwa msingi huo,” aliongeza.

Haya yanajiri wakati Rais William Ruto akiwa ameandikia mabunge waraka kuyahimiza yatekeleze mabadiliko ya katiba ili kuanzisha afisi ya kiongozi wa upinzani.

“Ninaamini wazo la afisi ya kiongozi wa upinzani ni ziada ya ile ya Wachache katika bunge, ikiwa na mantiki zaidi katika kuimarisha utawala, kutia nguvu usimamizi na kukuza demokrasia,” inasema barua ya Rais Ruto kwa Bunge.

Hata hivyo, Rais anahisi kwamba mabadiliko ya kuunda wadhifa huo yanaweza kufanywa bila nchi kushiriki kura ya maamuzi.

“Ni muhimu kwamba tujaribu kushughulikia mageuzi haya kwa njia ambazo hazitarejesha siasa za migawanyiko za kampeni ya kura ya maamuzi,” alionya kiongozi huyo wa nchi.

Hata hivyo, wakili wa masuala ya Kikatiba Bob Mkangi alisema kuwa kubuniwa kwa afisi hiyo ni zaidi ya kuiingiza katika katiba kwa kuwa itaathiri muundo mzima wa Bunge na Serikali Kuu na hivyo basi ni lazima ishirikishwe katika kura ya maamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 225 ya katiba.

“Kimuundo, inagusia utukufu wa Wakenya na inaathiri jinsi Bunge linavyohudumu. Haya ni mawili ya maeneo 10 ambayo Ibara 225 ya katiba inahitaji mabadiliko yaamuliwe kupitia kura ya maamuzi,” akasema Bw Mkangi.

Mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo alisema kwamba mjadala kuhusu kuanzishwa kwa mswada huo ni njama ya kumfanya Bw Odinga kutozingatia mipango yake ya kukosoa serikali.

“Iwapo kuna kitu kimoja ambacho Rais Ruto hangetaka kuona ni mababadiliko ya katiba. Mabadiliko yoyote ya katiba bila shaka yatakuwa kura ya maamuzi ya uongozi wa William Ruto. Hafai kuyakubali katika muhula wake wa kwanza iwapo anataka kutimiza ahadi zake za maendeleo. Kwa hivyo, mchakato unaweza kuanzishwa, na iwapo utaanzishwa, ni lazima ahakikishe umezimwa na bunge,” akasema Bw Bigambo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Naam, sekta ya viwanda ipewe uzito

Mashabiki wa soka jijini Kisumu wapata utamu wa Kombe la...

T L