• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Raila asema hatachoka kudai haki na kupigania maisha bora ya raia

Raila asema hatachoka kudai haki na kupigania maisha bora ya raia

NA WANDERI KAMAU

SHUGHULI zilitatizika jijini Nairobi na baadhi ya maeneo nchini baada ya kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga kuongoza maandamano ya kupinga serikali.

Bw Odinga alitangaza kuwa atakuwa anaongoza maandamano kama hayo kila Jumatatu – hatua ambayo itapandisha joto la kisiasa na taharuki nchini.

Akiwahutubia wafuasi wake katika maeneo mbalimbali jijini Nairobi, Bw Odinga alisema kuwa hawatalegeza juhudi zao za kuishinikiza serikali hadi pale matakwa yao yatakapozingatiwa.

Akiandamana na vigogo wenzake -Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (Narc-K) na aliyekuwa waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa kati ya wengine- Bw Odinga alisema wakati umefika wa serikali ya Kenya Kwanza “kukabiliwa kwa vitendo badala ya matamshi”.

“Tutakuwa tukifanya maandamano kila Jutatatu hadi pale matakwa yetu yatakapozingatiwa,” akasema Bw Odinga huku akishangiliwa na maelfu ya wafuasi wake.

“Wakenya wamechoshwa na ugumu wa maisha na uongozi wa serikali isiyowajali,” akaongeza Bw Odinga.

Tangazo hilo ni urejeo wa maandamano kama hayo yaliyoshuhudiwa 2017, maarufu kama Jumatatu ya Machozi, ambapo Bw Odinga aliongoza juhudi za kupinga ushindi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Baadhi ya masuala ambayo Bw Odinga anaitaka serikali kushughulikia ni kupunguza gharama ya maisha, kufungua seva za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuanza upya kwa mchakato wa kuunda jopo litakalowateua makamishna wapya wa IEBC kati ya mengine.

Bw Odinga ameshikilia kuwa Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua hawakushinda kihalali kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9 mwaka uliopita.

Hapo jana Jumatatu, wafanyabiashara jijini Nairobi na maeneo mengine nchini walilazimika kufunga biashara zao kwa kuhofia athari za maandamano hayo.

Jijini Nairobi, maduka mengi yalifungwa siku nzima huku barabara nyingi zikibaki bila watu ama shughuli zozote.

Polisi waliwekwa katika barabara kuu za kuingia katikati ya jiji kuwazuia wafuasi wa Bw Odinga kuingia jijini, kwani alikuwa ametangaza angewahutubia katikati ya jiji na baadaye kuelekea Ikulu ya Nairobi “kuukomboa ushindi wao”.

Nyakati za asubuhi, maduka mengi jijini hayakuwa yamefunguliwa kama kawaida, wafanyabiashara wengi wakihofia kuwa huenda waandamanaji wakayatumia kuharibu na kupora biashara zao.

Polisi walilazimika kukabiliana na baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuingia katikati ya jiji kutoka katika eneo la Kibra kwa kuwarushia vitoa machozi.

Katika barabara ya Moi Avenue, baadhi ya wafanyabiashara walikuwa katika hali ya kungoja kuona jinsi hali ingekuwa.

Mwendo wa saa tatu, polisi waliwakamata watu wanne nje ya Mahakama ya Upeo. Polisi pia waliwakamata vijana kadhaa waliokuwa wamekusanyika nje ya Jengo la KICC.

Vijana hao walikuwa miongoni mwa waandamanaji waliokuwa wameanza kukusanyika katika jengo hilo, kwani Bw Odinga alikuwa amewatangazia wafuasi wake kuwa hapo ndipo angewahutubia.

Katika makazi ya kibinafsi ya Bw Odinga mtaani Karen, walinzi wa kibinafsi waliweka ulinzi mkali baada ya baadhi ya wafuasi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kutishia kuyavamia.

Shughuli za kibiashara jijini zilisimama mwendo wa saa nne unusu, baada ya makabiliano baina ya polisi na waandamanaji kuanza rasmi.

Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa ni Barabara ya Ring Road (iliyo katika mtaa wa Kilimani), mzunguko wa Mochari ya City, mzunguko wa Ngara kati ya maeneo mengine. Polisi pia waliwarushia vitoa machozi viongozi wa Azimio waliokuwa wakijaribu kuingia katika KICC.

Seneta Edwin Sifuna wa Nairobi alirushiwa vitoa machozi pamoja na wafuasi wake walipofika katika jumba la KICC.

Ikizingatiwa kuwa makabiliano hayo yalikuwa yakiendelea katika sehemu nyingi jijini, mtu mmoja alipigwa risasi katika Soko la Toi na kujeruhiwa, ambapo alikimbizwa hospitalini.

Wakati patashika hiyo ilipokuwa ikiendelea, baadhi ya viongozi wa Azimio walifanya kikao na wanahabari katika majengo ya Bunge, ambapo walikashifu “ukatili” uliokuwa ukiendeshwa na polisi dhidi yao.

Wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki) na Junet Mohamed (Suna Mashariki), walitaja maandamano hayo kuwa “kionjo tu”.

“Huu ni mwanzo tu. Mengi yaja,” akasema Bw Owino.

Wakati huu wote, Bw Odinga hakuwa amejitokeza licha ya wafuasi wake kukabiliana na polisi.

Viongozi wa Azimio (akiwemo Bw Odinga) walielekea katika hoteli ya Serena, walikokuwa wametarajiwa kuwahutubia wanahabari, baada ya kufanya kikao cha muda mfupi

Ilitajwa kuwa baada ya kikao hicho, Bw Odinga angeanza kuongoza vigogo wenzake kuelekea katikati ya jiji.

Hata hivyo, kizaazaa kilizuka mwendo wa saa nane, msafara wa Bw Odinga ulipokuwa ukiondoka katika hoteli hiyo kuelekea katikati ya jiji.

Polisi walilazimika kuwarushia viongozi hao vitoa machozi. Polisi walitumia malori makubwa ya kurusha maji ya kuwasha ngozi kuwazuia vigogo hao na wafuasi wao kuingia katikati ya jiji.

Vigogo hao walijaribu kutumia njia mbadala baada ya polisi pia kuziba Kenyatta Avenue.

Baada ya kuzuiwa kabisa kuingia katikati ya jiji, msafara wao ulielekea katika uwanja wa Kamukunji, walikowahutubia maelfu ya wafuasi wao.

Baada ya muda mfupi, walirushiwa vitoa machozi na kuelekea eneo la Pumwani. Baadaye walielekea katika eneo la Eastleigh, ambapo kwa mara nyingine, walirushiwa vitoa machozi na polisi.

“Lazima polisi wakome kutumia nguvu dhidi ya wafuasi wetu,” akasema Bw Odinga huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Baadaye alielekea katika mtaa wa Mathare.

Katika kaunti sita za eneo la Pwani, ambalo ni ngome ya kigogo huyo, shughuli ziliendelea kama kawaida wafuasi wakisusia miito ya maandamano.

  • Tags

You can share this post!

Aliyepokea 162,000 kimakosa akanunua ploti ajipata taabani

Fowadi Zlatan Ibrahimovic aweka rekodi ya kuwa mfungaji...

T L