• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
“Raila atapita hata bila kura za Mlima Kenya”

“Raila atapita hata bila kura za Mlima Kenya”

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe amewataka wakazi wa Mlima Kenya kuhakikisha kura zao zitachangia ushindi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akiongea kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen Jumanne usiku, Bw Murathe, hata hivyo, alielezea imani kuwa Bw Odinga atashinda hata bila kura za Mlima Kenya.

Alisema katika chaguzi za 2013 na 2017 waziri huyo mkuu wa zamani alikaribia kushinda ila hakuwa na uungwaji mkono kutoka eneo la Mlima Kenya.

“Katika matokeo ya chaguzi hizo Raila na Uhuru walipata karibu idadi sawa ya kura, yaani asilimia 50 kwa 50, ilhali Raila hakupata kura kutoka Mlima Kenya, “Hii ina maana kuwa wakati huu Raila akipata sehemu ya kura za Mlima Kenya atashinda kwa sababu bado anadhibiti ngome zake za zamani,” Bw Murathe akasema.

Aliongeza: “Nawaonya watu wetu wa Mlima Kenya kwamba watajilaumu ikiwa Raila atashinda urais bila mchango wa kura zao.”

Bw Murathe alisema Bw Odinga bado atapata kura nyingi eneo la magharibi, licha ya Naibu Rais William Ruto kufaulu kuvutia upande wake kinara wa ANC, Bw Musalia Mudavadi, na mwenzake wa Ford Kenya, Bw Moses Wetang’ula.

“Walidhani wangetoa eneo la magharibi kutoka kapu la Raila. Lakini ukweli ni kwamba Raila alimshinda Mudavadi nyumbani kwake Vihiga kwani gavana na diwani wake wote ni wa ODM,” akaeleza.

Katika uchaguzi mkuu wa 2013, Rais Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata kura 6, 173, 433 (asilimia 5.51) huku Bw Odinga akipata kura 5,340,546 (asilimia 43.7).

Katika matokeo ya urais ya uchaguzi wa 2017, Rais Kenyatta alipata kura 8,223, 369 (asilimia 54.17) ilhali Bw Odinga alipata kura 6,822, 812 (asilimia 44.94).

Hata hivyo, matokeo hayo yalifutiliwa mbalimbali na Mahakama ya Juu iliyoamuru uchaguzi wa urais urudiwe, ambapo Bw Odinga aliususia.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Rais Kenyatta anamuunga mkono Bw Odinga chini ya vuguvugu la Azimio la Umoja , inaloshirikisha zaidi ya vyama 15 vya kisiasa.

Akihutubu wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) wa ODM kwenye uwanja wa Kasarani, Nairobi, mnamo Februari 26, Rais Kenyatta alimsifia Bw Odinga akieleza kuwa ndiye anafaa kuchukua hatamu za uongozi wa taifa hili baada yake kustaafu.

“Yule kijana wangu atapata nafasi wakati atarekebisha tabia zake,” Rais Kenyatta akasema kumrejelea Dkt Ruto.

Jumamosi iliyopita, Bw Odinga aliidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais wa Azimio la Umoja katika hafla ya wajumbe (NDC) wa muungano huo iliyofanyika katika jumba la KICC mjini Nairobi.

Azma ya Bw Odinga ilipigwa jeki kufuatia hatua ya kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais na kutangaza kuwa atamuunga mkono waziri mkuu huyo wa zamani.

  • Tags

You can share this post!

Wito raia wavae maski wakisafiri

Wakazi waisifia serikali kwa kumwaga mamilioni kupanua...

T L