• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Raila avuna lawama za dosari za Jubilee

Raila avuna lawama za dosari za Jubilee

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amebebeshwa mzigo wa mapungufu ya serikali ya Jubilee, ambayo yanafanya safari yake ya Ikulu kuwa na changamoto.

Wachanganuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa handisheki kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta ilimvua mwanasiasa huyo sifa ya “mtetezi wa wanyonge” na badala yake akageuzwa “mradi” wa serikali.

“Nafasi ya Raila ya kuwa mkosoaji mkuu wa serikali na mtetezi sugu wa raia sasa imetwaliwa na Ruto ambaye amekosana na bosi wake. Hali hii kwa kisasi imeathiri kampeni za Bw Odinga,” anasema Bw Martin Andati.

Mchangunuzi huyo anaongeza kuwa kuchelewa kwa Rais Kenyatta kujitokeza waziwazi kumfanyia kampeni Bw Odinga katika ngome yake ya Mlima Kenya kumemkosesha mwaniaji huyo wa Azimio nguvu ya kuukwea Mlima Kenya.

“Hii ndio maana matokeo ya kura mbalimbali za maoni ikiwemo ya hivi punde iliyodhaminiwa na shirika la Nation, yanaonyesha kuwa umaarufu wa Raila eneo hilo ungali chini ya asilimia 50. Ruto bado ndio mwenye umaarufu mkubwa katika eneo hilo lenye kura nyingi,” Bw Andati anaeleza.

“Rais Kenyatta hana budi kwenda mashinani kuelezea wakazi wa Mlima Kenya ni kwa nini angetaka Raila awe mrithi wake na wala sio Ruto. Mikutano ambayo amekuwa akifanya na viongozi kutoka eneo hilo katika Ikulu za Sagana na Nairobi haitoshi,” anaongeza.

Inadaiwa kuwa hii ndio maana wagombeaji viti mbalimbali kwa tiketi ya Jubilee, kinachoongozwa na Rais Kenyatta, wanahepa kuweka picha za Bw Odinga katika mabango yao ya kampeni.

Hii ina maana kuwa wawaniaji hao wanahisi kwamba watapoteza uungwaji mkono endapo watajihusisha na Bw Odinga, licha ya kwamba chama cha Jubilee ni mshirika wake mkuu katika muungano wa Azimio.

Mbunge mmoja wa chama cha Jubilee aliambia Taifa Leo kwamba hali kama hii inatokea katika eneo la Mlima Kenya kwa sababu Rais Kenyatta hajatoa mwelekeo kwao.

“Tunataraji kuwa kiongozi wa chama chetu atapata nafasi ya kuzuru eneo ili atoe mwongozo kuhusu jinsi tutamuuza Raila,” akasema Mbunge huyo.

Rais Kenyatta pia anaonekana kushindwa kudumisha umoja miongoni mwa vyama tanzu ndani ya Azimio, hali ambayo imechangia vyama viwili kujiondoa.

Hii ni licha ya kwamba vyama hivyo, Maendeleo Chap Chap (MCC) na Pamoja African Alliance (PAA) vilijiunga na muungano huo kupitia chama cha Jubilee.

“Kujiondoa kwa vyama hivi viwili kumetoa taswira kwamba mambo sio shwari hata miongoni mwa vyama vilivyosalia ndani ya Azimio. Hii bila shaka itaathiri nafasi ya Bw Odinga,” anasema Bw Mark Bichachi.

“Rais Kenyatta kama mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio anapaswa kuitisha mkutano wa dharura ili kutatua changamoto zinazokabili muungano huu, endapo amejitolea kuhakikisha unashinda urais Agosti 9,” anashauri.

Maadui wa wa kisiasa wa Bw Odinga wakiongozwa na Dkt Ruto wamekuwa wakimlaumu kuhusu kukwama kwa Ajenda Nne Kuu.

“Rais alipoamua kufanya kazi na ndugu yake wa handisheki niliheshimu uamuzi wake. Raila na hao wengine aliowapa majukumu yangu ndio wamefeli,” Dkt Ruto akasema mjini Bungoma wiki iliyopita.

“Sababu halisi ya kupanda kwa gharama ya maisha ni usimamizi mbaya wa uchumi chini ya Uhuru na Raila ambao ndio wameshika usukani baada ya kutengwa kwa Ruto,” akasema Kinara wa ANC, Musalia Mudavadi.

Akihutubu katika sherehe za Leba Dei, Rais Kenyatta alikiri kuwa amekuwa akipata ushauri kutoka kwa Bw Odinga kuhusu namna ya kuendesha masuala ya serikali na kukabiliana na changomato zinazowazonga Wakenya.

Kukiri huko kunamfanya Bw Odinga kuwa miongoni mwa wanaolaumiwa kwa matatizo mengi wanayopitia Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

Karua, Mudavadi wapendwa zaidi kwa unaibu rais

Israeli motoni kwa kuua mwanahabari

T L