• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
KPA yashindwa kusimamisha kesi dhidi ya mkurugenzi mkuu

KPA yashindwa kusimamisha kesi dhidi ya mkurugenzi mkuu

NA BRIAN OCHARO

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (KPA) imepata pigo baada ya kushindwa kuzuia kusikilizwa kwa kesi ya kupinga uteuzi wa John Mwangemi kama kaimu mkurugenzi.

Mahakama ya Ajira ilikataa kusitisha kusikilizwa kwa kesi huku ikisema kuwa sababu zilizotolewa na KPA zilikuwa dhaifu.

Jaji Byram Ongaya alisema kuwa hatua ya KPA kutoa kigezo kwamba ilichelewa kukabidhiwa nakala ya malalamishi kutoka kwa mlalamishi, haikuwa na mashiko.

Mahakama ilisema kuwa pingamizi ya KPA inapotosha kwa sababu haikutokana na ukweli usiopingika kuhusu suala la kupewa kwa karatasi za mahakama.

Kesi ya kupinga kuteuliwa kwa Bw Mwangemi kama kaimu mkurugenzi mkuu wa KPA iliwasilishwa na shirika la Commission for Human Rights and Justice (CHRJ).

Lakini KPA ilipinga kesi hiyo ikisema kwamba CHRJ ilifeli kuwasilisha nakala za malalamishi kwa mawakili wa mamlaka hiyo ndani ya muda ulioagizwa na mahakama.

Kwa mujibu wa KPA, mlalamishi alipaswa kuwa amewapa mawakili wake stakabadhi hizo Julai 9, 2021.

“Kwa kukosekana kwa ruhusa ya kuendelea na kesi hii, mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii,” wakili wa KPA John Kinyanjui alisema.

Bw Kinyanjui pia aliteta kuwa mlalamishi anafaa kuadhibiwa kwa kukiuka maagiza ya mahakama kukosa, kupuuza na kukataa kuwasilisha stakabadhi zote kwa wakati.

Wakili huyo aliendelea kusema kuwa KPA haikupewa stakabdhi muhimu ya keshi hiyo kama vile hati ya kiapo.

“Ruhusa ya kuwasilisha kesi hiyo iliisha wakati CHRJ iliposhindwa kuwasilisha stakabadhi kwa wakati. Mlalamishi amedharua mahakama na hatakiwi kusikilizwa mbele ya mahakama hii ,” alisema.

Lakini mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo ikiitaja kuwa ni matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama.

“Notisi ya pingamizi la awali imebainika kuwa ni matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama kwa vile ilidhamiria kuweka dhima ya kudharau mahakama dhidi ya CHRJ,” Jaji Ongaya.

Aidha jaji huyo aliagiza pande zinazohusika katika mzozo huo kuchukua hatua za kusikilizwa kwa haraka kesi hiyo.

Kesi ya kupinga uteuzi wa Bw Mwangemi ilithibitishwa kuwa ya dharura mwaka 2021 na CHRJ ikapewa idhini ya kuiwasilisha rasmi.

Kupitia kwa mkurugenzi Julius Ogogoh, CHRJ inataka uteuzi huo ubatilishwe kabisa, ikisema ulifanywa kwa siri na hivyo kukiuka utaratibu unaohitajika wa kuajiri kama ilivyoainishwa chini ya Sheria ya KPA na Sheria ya Tume ya Utumishi wa Umma.

Bw Ogogo anahoji kuwa chini ya Sheria ya KPA, Waziri wa Hazina ya Kitaifa (CS) Ukur Yatani anastahili kufanya uteuzi huo kwa kushauriana na bodi ya wakurugenzi ya KPA.

Mlalamishi huyo pia anahoji kuwa bodi hiyo, ambayo ilipaswa kushauriana na CS kabla ya uteuzi huo kufanywa, haijaundwa ipasavyo.Muda wa mwenyekiti wa bodi na wanachama wengine watatu wa bodi hiyo ulimalizika Juni 5, 2021 lakini tangu hapo imebaki na wanachama wachache.

Kulingana na CHRJ, Bw Mwangemi hakutuma maombi ya wadhifa huo wala kuorodheshwa katika zoezi la awali la kuwasajili waliohojiwa.

“Wale walioteuliwa na kuohojiwa walikataliwa na Bw Yatani , ambaye amemteua Bw Mwangemi kiholela na kwa uzembe na kisiri,” Bw Ogogo alisema.

Mlalamishi analalamika kwamba uteuzi wa kisiri wa Bw Mwangemi uliwanyima waliohitimu na waliotimiza masharti na Wakenya wengine fursa ya kuajiriwa kisheria.

CHRJ linaitaka mahakama kutoa agizo la kupiga marufuku KPA kumshikilia Bw Mwangemi kama kaimu mkurugenzi mkuu wa shirika hilo na pia kutekeleza majukumu yake kama bosi wake.

Hata hivyo, KPA inataka kesi hiyo itupiliwe mbali ikiitaja kama matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama.

Bw Mwangemi aliteuliwa kuwa kaimu MD mnamo Julai 1.

Alichukua nafasi ya Rashid Salim.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KPA Mhandisi Rashid Salim (kulia) alipomkabidhi mamlaka John Mwangemi katika makao makuu ya KPA, Julai 1, 2021. PICHA | MAKTABA

Bw Salim alishikilia wadhifa huo kama kaimu kwa zaidi ya mwaka mmoja kufuatia kujiuzulu ghafla kwa Dkt Daniel Manduku kwa madai ya ufisadi mnamo Machi 28, 2020.

KPA imekuwa ikifanya kazi tangu Machi 28, 2020 bila mkurugenzi mkuu kwani harakati za awali za kuajiri zimeshindwa kutoa mgombea anayefaa kwa wadhifa huo.Mwisho

You can share this post!

UN yakerwa na mauaji ya raia 108 katika jimbo la Tigray...

Raila awahimiza Wakenya washirikiane bila kujali kabila,...

T L