• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Raila kujipata hali tata korti ikikataa ombi

Raila kujipata hali tata korti ikikataa ombi

NA BENSON MATHEKA

HUENDA mgombea urais wa muungano wa Azimio Raila Odinga akajipata kwenye hali tata Mahakama ya Upeo ikiamua uchaguzi wa marudio ufanyike ukisimamiwa na mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati.

Katika kesi yake ya kupinga ushindi wa William Ruto, Bw Odinga anaomba majaji kuagiza uchaguzi mpya wa urais ufanywe Bw Chebukati akiwa nje.

Bw Odinga anadai Bw Chebukati alivuruga uchaguzi wa 2017 uliobatilishwa na mahakama, na ikipatikana alirudia makosa hayo kwenye uchaguzi wa mwaka huu 2022 basi hafai kusimamia uchaguzi wa marudio.

Wachanganuzi wanasema iwapo ombi lake litakataliwa na mahakama, huenda Bw Odinga akajipata katika hali iliyomkumba mwaka wa 2017, alipokataa kushiriki uchaguzi wa marudio baada ya ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta kufutwa na mahakama.

“Raila alisusia uchaguzi wa marudio 2017 akisema hakutarajia matokeo tofauti kwa kuwa ulisimamiwa na tume iliyovuruga uchaguzi wa kwanza. Tunasubiri kuona iwapo atabadilisha nia mahakama ikikataa ombi lake kwenye kesi aliyowasilisha mwaka huu,” asema mtaalamu wa masuala ya uchaguzi wa Jumuiya ya Madola Wakili Tom Maosa.

Ingawa anasema kwamba maombi ya Bw Odinga na mazingira ya uchaguzi wakati huu ni tofauti na 2017, uamuzi wa majaji utakuwa wa mwisho.

“Iwapo itaamuliwa uchaguzi urudiwe na kusimamiwa na Bw Chebukati na Bw Odinga akatae kushiriki, wafuasi wake watakosa imani naye na itakuwa pigo kwa maisha yake ya kisiasa,” akasema Bw Maosa.

Mmoja wa mawakili wanaotarajiwa kuwakilisha Bw Odinga katika kesi yake ambaye aliomba tusitaje jina kwa wakati huu, aliambia Taifa Leo kwamba waziri mkuu huyo wa zamani anaheshimu utawala wa sheria na atakubali uamuzi wa mahakama.

  • Tags

You can share this post!

Omtatah adai kuna kura ziliachwa nje

Hasira wafanyakazi wa Mumias wakitaka mwekezaji atimuliwe

T L