• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Raila kuzuru Nyanza kura zikinukia

Raila kuzuru Nyanza kura zikinukia

NA RUSHDIE OUDIA

MGOMBEA urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga atafanya kampeni yake ya kipindi cha lala salama katika ngome yake maeneo ya Nyanza na Magharibi huku akitumai kuvutia wapigakura kuunga mkono azma yake.

Kulingana na msemaji wa serikali, Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga watazindua Kituo cha Meli Kisumu na pia kushuhudia uzinduzi rasmi wa Feri ya MV Uhuru II Wagon hapo kesho Jumanne.

Kuwepo kwa Kiongozi wa Taifa kunadhamiriwa kuimarisha hata zaidi uhusiano wake na Bw Odinga na pia kuhakikishia wenyeji kuwa atalikabidhi taifa kwa mshirika wake katika handisheki.

Huku ikiwa imesalia wiki moja tu kabla ya chaguzi za Agosti, Bw Odinga na timu yake ya kampeni wanajitahidi kwa kila hali kusaka kura eneo hilo.

Wagombea wanaowania kwa tiketi ya ODM wanatumai Bw Odinga atawafanyia kampeni ili kuwapiga jeki dhidi ya wagombea huru wanaowakosesha usingizi katika eneo la Nyanza.

Mpinzani wake mkuu, Naibu Rais William Ruto, ambaye ni mgombea urais wa UDA amefanya kampeni kadhaa katika ngome ya Bw Odinga, Nyanza na Magharibi na kuzua ushindani katika kampeni.

Huku akifanya kampeni yake ya mwisho, Bw Odinga atawarai wafuasi wake kumpigia kura kwa wingi ili kumwezesha kushinda kiti cha urais kinachoshindaniwa vikali baada ya kujaribu mara nne bila kufanikiwa kuingia ikulu.

Mgombea urais wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na wandani wake wamewaonya wapiga kura kwamba kumchagua bila idadi kubwa ya wabunge kutamfanya rais asiye na nguvu.

Kulingana na ratiba yake rasmi ya kampeni iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Muungano huo, Bw Junet Mohammed, Azimio itakuwa Kisii kesho Jumanne ambapo Bw Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua watafanya mkutano katika uwanja wa Kisii.

Jumatano, wawili hao watakuwa katika Uwanja wa Bukhungu, Kakamega na mnamo Alhamisi, Agosti 4, watakuwa Kisumu kwa mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Mamboleo.

Baada ya kuafikiana na ngome zake maeneo ya Nyanza na Magharibi, mwaniaji urais wa Azimio atazuru Mombasa kuwarai wafuasi wake katika uwanja wa Tononoka.

Kisha ataelekea kwenye mkutano wa mwisho katika Uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Moi, Kasarani, Nairobi mnamo Jumamosi.

Wachanganuzi hata hivyo, wanachukulia mikutano ya mwisho iliyopangwa na Bw Odinga kama hatua ya kuwashambulia washindani wake na mpango mkuu wa kuwazika “wakaidi” wanaoshindana na wagombea wa ODM kwa kupigia debe mtindo wa suti wa upigaji kura na vilevile kuwachochea wapiga kura kutoka ngome yake kujitokeza kwa wingi.

  • Tags

You can share this post!

Wagombeaji ugavana wakaidi wito wa Raila

Mwenyekiti wa Bodi ya NMG ahimiza amani

T L