• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Raila Odinga atangaza rasmi kuwania urais 2022

Raila Odinga atangaza rasmi kuwania urais 2022

Na SAMMY WAWERU

NI rasmi sasa kiongozi wa ODM, Raila Odinga atakuwa debeni kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao, 2022. 

Waziri huyo Mkuu wa zamani alitoa tangazo hilo Ijumaa, katika kongamano la vuguvugu la Azimio la Umoja, analoliongoza.

Akihutuu katika Uwanja wa Kimataifa wa Safaricom, Kasarani, jijini Nairobi, Bw Raila aliorodhesha ajenda 10 ambazo serikali yake itazipa kipau mbele endapo atafanikiwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Zinajumuisha, Inua Jamii ambapo kiongozi huyo wa upinzani anasema analenga kuhakikisha kila familia isiyo na kazi inakuwa na pesa mfukoni, Babacare-afya kwa wote, Kazi kwa Wote, Uchumi kwa Akina Mama, Fukuza Njaa, kati ya nyinginezo.

“Mimi ni mwana wa Kenya, mtetezi wa ukombozi na mhudumu wa wananchi kwa muda wa miaka 50. Sijutii niliyopitia nikipigania uhuru wa nchi hii,” Bw Raila akaelezea, waliokongamana wakishangilia jitihada zake.

Akiuza sera zake kuwania urais mwaka ujao, hakusita kurejelea mapatano kati yake na Rais Kenyatta, maarufu kama Handisheki.

Wawili hao Machi 2018, walitangaza kuzika tofauti zao na kuahidi kuunganisha taifa, hatua ambayo imepelekea kiongozi huyo wa upinzani kushirikiana kwa karibu na Rais.

“Lazima nimpongeze na kumshukuru ndugu yangu, Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta kufuatia uzalendo wake kuanzisha mjadala wa Handisheki. Inachukua hatua za jasiri kuamkuana na mpinzani wake,” Raila akasema. 

Raila 2017 aligombea urais mara ya nne, japo akabwagwa na Rais Kenyatta aliyewania kuhifadhi kiti chake pamoja na naibu wake, Dkt William Ruto.

Chini ya muungano wa Nasa, Raila alipinga ushindi wa wawili hao katika mahakama ya juu zaidi ambapo matokeo yalifutiliwa mbali, na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuandaa marudio Oktoba 26, 2017.

Nasa hata hivyo haikushiriki huku ngome za ODM zikishuhudia ghasia na vurumai. Kongamano la Azimio la Umoja lilihudhuriwa na mamia na maelfu ya watu, wakiwemo baadhi ya maafisa wakuu serikalini, mawaziri, magavana, maseneta na wabunge.

Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed alisema mkutano huo ni wa kimataifa, kufuatia mwaliko wa wageni kutoka nje ya nchi.

Aliyekuwa rais wa Nigeria, Bw Olusegun Obasanjo ni miongoni mwa wageni mashuhuri waliohudhuria.

“Tumezuru karibu kila kona ya nchi kuhubiri Azimio la Umoja. Tunataka Wakenya watangamane kwa njia ya amani, bila kuangalia kabila wala rangi,” Bw Junet akasema.

Hali ya usalama iliimarishwa ndani na nje ya uwanja wa Kasarani, maafisa wa usalama wakishika doria.

Dkt Ruto ndiye mpinzani mkuu wa Raila Odinga, katika uchaguzi ujao.  Ruto ametangaza kuwania urais kupitia UDA.

Vinara watatau wa One Kenya Alliance (OKA) hawakuhudhuria kongamano hilo, licha ya kupata mwaliko.

Wanajumuisha Mabw Musalia Mudavadi wa ANC, Moses Wetangula (Ford-Kenya) na Kalonzo Musyoka wa Wiper.

Kiongozi wa KANU na ambaye ni kati ya vinara wa OKA alihudhuria. Itakumbukwa kwamba Kalonzo, Mudavadi na Wetangula walikuwa vinara wenza wa Raila katika muungano wa Nasa.

Katika uchaguzi wa 2017, Bw Kalonzo alikuwa mgombea mwenza wa Raila.  Nasa hata hivyo ilisambaratika, OKA ikinyooshea Raila kidole cha lawama kwa kile wanadai ni “kutusaliti na kutoheshimu mkataba wa makubaliano kati yetu”.

Muungano huo haujatangaza ni nani atakayepeperusha bendera yake kuwania urais mwaka ujao.

You can share this post!

Kaunti kusaidia manesi wanaotaka kwenda ulaya

Shirikisho la Hoki Afrika latangaza washiriki wa Kombe la...

T L