• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wahubiri wahimiza kampeni za heshima

Wahubiri wahimiza kampeni za heshima

Na JUMA NAMLOLA

NAIBU Rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga, wameonywa dhidi ya kutumia kampeni zao za kusaka kura kuzua ghasia mwaka 2022.

Viongozi mbalimbali wa makanisa wanasema ni lazima kila anayetaka uongozi atumie lugha ya unyenyekevu, na kukosoa sera za mwenzake bila kuonekana kuchochea wananchi.

Bila kuwataja wawili hao kwa majina, viongozi waliozungumza wakati wa sherehe za Krismasi, walisema kampeni za uchaguzi Mkuu ujao hazifai kutumiwa kuligawa taifa.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Jackson Ole Sapit, alitahadharisha viongozi hao wa kisiasa akisema kampeni hazifai kutumiwa kuwagawa wananchi.

“Tunawaonya wale wanaotafuta kura, wasiwagawanye Wakenya kwa misingi ya kikabila, au tofauti nyingine zozote,” akasema.

Aliwataka watu waheshimu misimamo ya wengine, na kutotumia kampeni kueneza chuki miongoni mwa wananchi.

“Nahimiza tusiwe na ule mtindo ambapo mwanasiasa asipokubaliana na maoni ya mwingine, wanakorofishana na kuzua vurugu. Tuingie kwenye kampeni za uchaguzi tukiwa timamu na tufanye mwaka 2022 kuwa wenye uchaguzi wa amani,” akasema.

Akizungumza wakati wa misa ya Krismasi mjini Kisumu, Mtawa Mary Awino alikumbusha vigogo wa kisiasa kwamba, nchi inakoelekea, hawapaswi kutoa matamshi yanayoweza kuitumbukiza taifa kwenye machafuko.

“Tunaelekea kwenye uchaguzi mwaka 2022. Ujumbe wetu kama viongozi wa kidini ni kuwahimiza wanasiasa wasitoe matamshi yanayoweza kututenganisha,” akasema Mtawa Awino.

Bw Odinga na Dkt Ruto wamekuwa wakitupiana cheche za maneno kuhusu sera zao za kiuchumi, pamoja na ahadi nyinginezo ambazo kila mmoja amekuwa akitoa kwa wananchi.

Isitoshe, wawili hao ndio wako kifua mbele kwenye kinyang’anyiro hicho cha kumtafuta mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye anatarajiwa kustaafu mwaka ujao baada ya kuhudumu kwa mihula miwili ambayo inakubalika kikatiba.

“Uchumi wa Bottom Up yafaa utupwe kwenye takataka. Hakuna chochote kama Bottom Up unapozungumzia masuala ya uchumi. Utatumiaje wilbaro au mkokoteni kuimarisha uchumi wa wananchi?” aliwahi kuuliza Bw Odinga.

Naye Bw Ruto amekuwa akimtaja Bw Odinga kuwa mganga akiongeza kuwa hasemi ukweli kuhusu Sh6,000 anazoahidi kutoa kwa familia masikini zisizokuwa na kazi.

“Huyu mjamaa anatuambia eti kuna trickle-down. Ni uganga gani atafanya safari hii, ambao mfumo huu wa uchumi umeshindwa kufanya kwa karibu miaka 60 iliyopita?” akauliza Dkt Ruto.

Majibizano haya wakati mwingine yamekuwa yakichukua mkondo hatari, ambapo wafuasi wa wawili hao wamekuwa wakirushiana kejeli na hata vitisho.

Viongozi wa makanisa wanasema raia wengi hawajui kutofautisha maneno ya siasa na chuki halisi.

Wakati huo huo, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Mombasa, Martin Kivuva, aliwatahadharisha wananchi dhidi ya kuchagua viongozi kwa misingi ya pesa.

Alionya kuwa wanasiasa wanaowahonga wakati wa kampeni, hawaaminiki kuwafanyia raia maendeleo.

“Kama utachagua kiongozi kwa sababu amekupa pesa, atakapoingia hatakujengea ile barabara unayotaka. Jukumu lake la kwanza litakuwa ni kurejesha pesa alizotumia kukuhonga,” akasema.

Kauli za viongozi hao wa makanisa zinajiri wakati Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, inatarajiwa kuchapisha tarehe ya Uchaguzi Mkuu ujao kwenye Gazeti Rasmi la Serikali Januari 19.

Baada ya hapo, watumishi wa serikali watatarajiwa kujiuzulu nyadhifa zao kabla ya Februari 9, iwapo wanapanga kuwania nyadhifa za kisiasa Agosti 9, 2022.

You can share this post!

West Ham wateremka zaidi katika jedwali la EPL baada ya...

Mswada tata wa vyama kujadiliwa Jumatano

T L