• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Mswada tata wa vyama kujadiliwa Jumatano

Mswada tata wa vyama kujadiliwa Jumatano

IBRAHIM ORUKO na DAVID MWERE

KAMATI ya Bunge Kuhusu Sheria imekubali malalamishi ya umma na kuamua kupunguza muda ambao vyama vya siasa vitaweka mikataba ya muungano na Ofisi ya Kusajili Vyama vya Kisiasa (ORPP), iwapo Mswada uliowasilishwa bungeni utapitishwa.

Mojawapo ya marekebisho yaliyopendekezwa kwenye mswada wa sheria ya vyama vya kisiasa, 2021, ni kupunguzwa kwa muda huo kutoka miezi sita hadi miezi mitatu.

Kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Mathioya, Muturi Kigano, pia imeelekeza macho yake katika kifungu cha 18 cha Mswada huo ambacho kikipitishwa kitavipa vyama vya Siasa siku 120 hadi tarehe ya uchaguzi mkuu kuwasilisha majina ya wanachama wake na taarifa ya mali na madeni yao.

Hata hivyo, kamati hiyo inapendekeza muda wa uwasilishaji wa majina ya wanachama upunguzwe kutoka siku 120 hadi 90.

Marekebisho hayo huenda yakatuliza hisia za wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais, William Ruto ambao wamepinga vikali Mswada huo wakidai huenda sheria hiyo inayopendekezwa ni njama ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuwafanya viongozi wanne wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kumuunga mkono kinara wa ODM, Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022.

Walio katika vyama vya kisiasa visivyo na umaarufu pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu marekebisho hayo huku wakionya kwamba, huenda mswada huo ukawafungia nje kufanya mipango ya muungano kwani miezi sita ni muda mrefu sana.

Mbunge wa Lugari, Ayub Savula, ambaye pia aliwasilisha pendekezo la kupunguza muda wa uwasilishaji majina ya wanachama alisema kuwa mswada huo utavifungia vyama vitakavyotaka kuunda muungano.

You can share this post!

Wahubiri wahimiza kampeni za heshima

Wakenya washerehekea Krismasi sehemu mbalimbali

T L