• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Rais akabidhiwa fimbo na wazee kuongoza Mlima Kenya

Rais akabidhiwa fimbo na wazee kuongoza Mlima Kenya

NA MWANGI MUIRURI

WAZEE wa jamii za Mlima Kenya, Jumamosi, walimpa kibali Rais Uhuru Kenyatta kuziongoza jamii hizo kwa muda wa miaka mitano ijayo, kwenye kikao kilichofanyika katika Ikulu ya Nairobi.

Rais Kenyatta alikabidhiwa fimbo ya uongozi mnamo No – vemba 2012 kutoka kwa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, hali iliyomfanya kuwania urais mwaka 2013 na 2017 kwa niaba ya jamii hizo.

“Mnamo 2012, tulimkabidhi fimbo mbili maalum zinazojulikana kama “muthiigi” (kwa lugha ya Gikuyu) ambazo huwa ishara ya kukubali kuchukua uongozi. Hizo si fimbo za kawaida kwani huwa zimefanyiwa matambiko. Vile vile, huwa zimeambatanishwa na vifaa maalum vya uongozi,” akasema mwenyekiti wa Baraza la Jamii ya Agikuyu, Bw Wachira Kiago, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Moja ya fimbo hizo huashiria imani kwa Mungu mmoja huku fimbo ya pili ikiashiria roho za mababu wa jamii hiyo (ngomi).

Ili kuhitimu kukwezwa kiwango hicho cha uongozi, lazima mtu awe mwanamume, huku kitindamimba wake mwanamume awe amepashwa tohara.

Kiongozi huyo lazima pia aungwe mkono na wazee wa viwango viwili kwenye mpangilio wa kimamlaka wa wazee katika jamii hizo.

Hata hivyo, kauli ya mwisho hutolewa na ngazi ya juu zaidi ya wazee kiitwacho ‘Arathi’ (Manabii).

“Kundi hilo la wazee huwa linamchunguza na kumpiga msasa anayekabidhiwa fimbo hizo kuhusu ikiwa amejihusisha katika vitendo vibaya kama mauaji, urogi, ubakaji au dhuluma za kimapenzi. Ikiwa atabainika kuhusika katika mojawapo ya vitendo hivyo, hawezi kuidhinishwa kama kiongozi,” akasema Bw Kiago.

Alieleza kuwa kabla ya fim – bo hiyo kukabidhiwa kiongozi husika, huwa inapelekwa kuombewa kwa siku 40 katika Mlima Kenya. Jamii ya Agikuyu inaamini kuwa Mungu wao (Ngai) anaishi katika mlima huo.

Ikizingatiwa walifanya hivyo miaka kumi iliyopita, wazee hao hawakurejelea utaratibu huo mara hii kwani walikuwa tayari washakubaliana kuwa “Rais Kenyatta bado ni mchanga na hajaonyesha tatizo lolote kwenye utekelezaji wa majukumu yake.” Alieleza kuwa ni sababu hiyo ambapo wazee waliamua kumuunga mkono kwa kauli moja.

Kando na fimbo hizo mbili, Rais Kenyatta pia alikabidhiwa upanga ambao unampa nguvu ya kuchinja mbuzi za kuendesha matambiko na pembe kumpa nguvu kuunganisha jamii hiyo pamoja.

“Rais Kenyatta vile vile alikabidhiwa mkuki na sime ambazo zinampa nguvu ya kuwaita watu wake kushiriki kwenye vita,” akasema.

Mara tu baada ya kupewa kibali hicho, Rais Kenyatta alipuliza pembe hiyo kama ishara ya kuzishinikiza jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA) kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kuwania urais,” akaeleza.

Duru kutoka Ikulu zilieleza Rais Kenyatta pia alichukua nafasi hiyo kuwaelezea wazee hao sababu zilizomfanya kutofautiana vikali na Naibu Rais William Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Baba achezea wagombeaji ODM kwa kutoa tiketi moja kwa moja

Wanawake, viongozi wa kidini wapongeza Karua

T L