• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Rais Odinga: Mwanzo mpya au ahadi hewa?

Rais Odinga: Mwanzo mpya au ahadi hewa?

NA WANDERI KAMAU

JE, taswira ya urais wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga, itakuwa vipi ikiwa ataibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022?

Hilo ni miongoni mwa maswali ambayo yameibuka, kufuatia ahadi ambazo amekuwa akitoa kwa Wakenya kwenye mikutano mbalimbali ambayo amefanya katika sehemu tofauti nchini.

Ingawa Bw Odinga hajatangaza rasmi azma yake kuwania urais mwaka ujao, anatarajiwa kutangaza nia yake Desemba 9, kwenye mkutano mkubwa ambao utafanyika jijini Nairobi. Kama vigogo wale wengine, Bw Odinga ametoa msururu wa ahadi, baadhi zikiwa ‘msaada’ wa Sh6,000 kila mwezi kwa kila familia ambayo jamaa zake hawana ajira rasmi.

Bw Odinga pia ameahidi kubuni mamilioni ya nafasi za ajira kwa vijana, kuboresha mfumo wa ugatuzi ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali ya Kitaifa kwa kaunti zinawafaa wananchi mashinani kati ya nyingine.

Swali ni: Atayatimiza hayo yote ikiwa ataibuka mshindi na kuapishwa kama rais wa tano wa Kenya? Kulingana na wadadisi wa siasa, kuna uwezekano Bw Odinga kujipata katika hali sawa na ulipojipata utawala wa Jubilee, baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa 2013.

Wadadisi wanasema utawala huo ulijipata pabaya baada ya kutoa ahadi nyingi kwa Wakenya, baadhi zikiwa kutoa vipakatalishi (laptops) kwa kila mwanafunzi atakayejiunga na Darasa la Kwanza.

“Ukitathmini kwa kina, Wakenya wengi walivutiwa sana na ahadi ambazo Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walitoa kwao. Hilo ni kando na mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Kwa mfano, ahadi ya ‘kuwahamisha kutoka analogi hadi mfumo wa dijitali’ uliwavutia sana vijana na watu wa umri wa makamo,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, mdadisi huyo anasema kuwa licha ya ahadi hizo, utawala wa Jubilee ulishindwa kutimiza baadhi yazo.

GHADHABU

Anasema kushindwa huko ndiko kumejenga ghadhabu miongoni mwa Wakenya wengi, hasa waliowapigia kura Rais Kenyatta na Dkt Ruto, kwani wanahisi “wamewasaliti.” “Baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa 2017, Jubilee iliahidi

kutekeleza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo. Ajenda hizo zilijumuisha uboreshaji wa sekta ya ujenzi, afya bora kwa wote, utoshelevu wa chakula na ukuzaji wa viwanda. Licha ya ahadi hizo, haijafanikiwa kutimiza nyingi yazo. Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini bado kiko kuu.

Huduma za afya bado ni ghali. Mpango wa kujenga nyumba ni kama umekwama huku viwanda vichache vilivyopo vikishindwa kufikia malengo yaliyoku – wepo,” akasema.

Ili kuepuka hayo, wadadisi wanasema ni lazima Bw Odinga awe mwangalifu ili asitoe ahadi ambazo huenda baadaye zikageuka kuwa ‘laana’ kwake.

Kwa mfano, wanaeleza huenda ahadi ya kutoa ‘usaidizi’ wa Sh6,000 kwa kila familia ambayo haina mtu asiye ajira rasmi ikakosa kutimika kutokana na hali mbaya ya uchumi wa nchi.

“Hiyo ni ahadi anayopaswa kutahadhari sana kutoa kwa wafuasi wake na Wakenya kwa jumla.

Utimizaji wa ahadi kama hizo huhitaji mikakati kabambe ya kiuchumi. Je, amewashirikisha wanauchumi ili kutathmini ikiwa jambo hilo litawezekana?” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Hata hivyo, anasema kuwa ikiwa Bw Odinga atafanikiwa kumbwaga Dkt Ruto na kuibuka mshindi kwenye uchaguzi huo, basi huo huenda ukawa mwanzo mpya kwa Kenya.

“Atakuwa ametimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuwa rais wa Kenya,” akaeleza Bw Mutai.

 

You can share this post!

Kalonzo kimya ngome yake ikivamiwa

Ashtakiwa kuiba mkokoteni aliodai ulitwaliwa na kanjo

T L