• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Ruto aanza kazi

Ruto aanza kazi

Na BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto jana Jumanne alianza kutimiza mara moja ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi, punde tu baada ya kuapishwa kuwa rais wa tano wa Kenya.

Kwenye hotuba yake ya kwanza kama rais katika uwanja wa michezo wa Kasarani jijini Nairobi, Rais Ruto aliwafaa wakazi wa Pwani aliagiza shughuli za bandari kurejeshwa Mombasa mara moja kutoka Nairobi na Naivasha.

“Adhuhuri ya leo, nitatoa maagizo ya kuondoa bidhaa na shughuli zingine katika Bandari ya Mombasa nilivyoahidi Wakenya,” Dkt Ruto alisema akieleza kuwa hatua hiyo itarejesha maelfu ya kazi katika jiji la Mombasa.

Kumekuwa na vilio miongoni mwa wakazi wa Pwani kufuatia hatua ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuhamisha shughuli za uondoaji mizigo kutoka bandari ya Mombasa hadi Nairobi na Naivasha. Hatua hiyo ilifanya biashara nyingi zilizotegemea Bandari ya Mombasa kuporomoka na maelfu ya watu kupoteza ajira.

Rais Ruto pia alitimiza ahadi yake kwa kuteua majaji 6 waliokataliwa na Bw Kenyatta: “Ili kudhihirisha kujitolea kwangu katika kuheshimu uhuru wa Mahakama, leo adhuhuri nitawateua majaji sita ambao walipendekezwa na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) kuteuliwa katika Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu. Kesho, nitaongoza kuapishwa kwao ili waanze kazi ya kuhudumia Wakenya.”

Baadaye jioni, Rais Ruto alitekeleza ahadi hiyo kwa kuwateua majaji Aggrey Muchelule, George Odunga, Weldon Korir na Profesa Joel Ngugi kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa huku Evans Makori Kiago na Judith Omange wakiteuliwa majaji wa mahakama ya mazingira na ardhi.

Ili kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha polisi wanatekeleza majukumu yao kwa njia huru bila kuingiliwa kisiasa, Rais Ruto alisema amechukua hatua zifaazo kuhakikisha Idara ya Polisi inajisimamia kifedha badala ya kutegemea bajeti ya Afisi ya Rais.

“Ninapowahutubia hivi sasa, nimeagiza kuanaliwa kwa mfumo wa kuhakikisha Idara ya Polisi inajitegemea kifedha kwa kuhamisha bajeti yao kutoka Afisi ya Rais na kufanya Inspekta Jenerali wa polisi kuwa msimamizi wa fedha hizo,” alisema akieleza kuwa polisi wakiwa na uhuru wa kifedha wataweza kutekeleza majukumu yao kwa njia bora zaidi na bila ubaguzi.

Kuhusu bei ya juu ya bidhaa za chakula, Rais Ruto alisema japo suala hilo linahitaji suluhu la muda mrefu, hatua yake ya kwanza ni kupunguza bei ya mbolea ili kuwezesha wakulima kuzalisha chakula zaidi. Ili kutimiza hilo, alipunguza bei za gunia ya mbolea ya kilo 50 kutoka Sh6,500 hadi Sh3,500 kuanzia wiki ijayo.

Kiongozi wa nchi alisema katika kutimiza ahadi yake ya kuwezesha biashara ndogo, atabuni hazina ya mahasla na kuweka mikakati ya kufanikisha mazingira ya biashara, pamoja na kupunguza idadi ya leseni za kibiashara pamoja na kukomesha kuhangaishwa kwa wafanyibiashara ndogo.

“Tutatekeleza Hazina ya Mahasla itakayokuwa ya kupatia biashara ndogo na za kati mtaji kupitia vyama, vyama vya akiba na mikopo na vyama vya ushirika,” alisema.

Kampeni yake ya uchaguzi mkuu uliopita ilikita katika mfumo wa kujenga uchumi kwa kuwezesha biashara ndogo kujiimarisha.

Rais Ruto pia alisema ataunda jopo kukusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu wa CBC, ambao umezua mjadala miongoni mwa washikadau, na akahakikishia Wakenya kwamba maoni yao yatazingatiwa kabla ya mwaka ujao wanafunzi watakapokuwa wakijiunga na kidato cha kwanza chini ya mfumo wa 8-4-4 na Gredi ya Saba chini ya mtaala huo mpya.

Maagizo mengine aliyotoa Rais Ruto siku yake ya kwanza kazini ni kuongezwa kwa bajeti ya Idara ya Mahakama, kuhakikisha machifu na maafisa wengine wa utawala wa mikoa hawatumiki kisiasa, ujenzi wa masoko 20 mapya jijini Nairobi na kukomeshwa kwa CRB kusajili wanaoshindwa kulipa mikopo kiholela, akisema kutakuwa na mfumo bora wa kufanya hivyo.

Pia alitangaza mpango wa ujenzi wa nyumba 250,000 kila mwaka pamoja na serikali kulipa haraka iwezekanavyo madeni inayodaiwa na wafanyibiashara.

  • Tags

You can share this post!

Marais waisifia Kenya kwa kuendeleza demokrasia, amani

TAHARIRI: Ewe Rais Ruto utamfaa sana raia ukizitimiza ahadi

T L