• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Ruto afinya marafiki zake hadi nyumbani

Ruto afinya marafiki zake hadi nyumbani

NA LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto huenda akasababisha washirika wake kukosa idadi kubwa ya wabunge baada ya chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kusimamisha wawaniaji katika ngome zao.

Orodha ya wawaniaji viti iliyochapishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inaonyesha kuwa chama UDA kimesimamisha wawaniaji hadi katika maeneobunge ya nyumbani kwa washirika wake wakuu.

Washirika wake wakuu ambao Dkt Ruto amepelekea ushindani nyumbani ni pamoja na Musalia Mudavadi (Vihiga na Kakamega), Moses Wetangula (Bungoma na Trans Nzoia), Amason Kingi (Kilifi), William Kabogo (Kiambu) na Mwangi Kiunjuri (Laikipia).

Hiyo inamaanisha kuwa huenda wawaniaji wa ubunge wa Kenya Kwanza wakagawanya kura na kutoa mwanya kwa wapinzani kupenya na ushindi.

Nyumbani kwa Bw Mudavadi katika Kaunti ya Vihiga, UDA kimesimamisha wawaniaji katika maeneobunge manne kati ya matano.

Kati ya maeneo hayo ni Sabatia, nyumbani kwa Bw Mudavadi, ambako UDA kimesimamisha Clement Logova Sloya kuwania ubunge eneo la Sabatia. Bw Sloya anamenyana na Emmanuel Ayodi Lusigi wa ANC.

UDA pia kina mwaniaji wa useneta Vihiga, Jackson Swadi Kedogo ambaye anapambana na Enosi Butiko wa ANC pamoja na Mwanamke Mwakilishi, Violet Bagada Afandi, anayemenyana na Beatrice Kahai Adagala wa ANC.

Katika Kaunti ya Bungoma, UDA kimesimamisha wawaniaji katika maeneobunge manane kati ya tisa kumenyana na wale wa Ford-Kenya.

Wawaniaji wa UDA Bungoma ni Sitati Daniel Wanyama (Webuye Magharibi), Masibo Aineah Muyundo (Webuye Mashariki), Kikuyu Sabastian Mukuzi (Tongaren), Chesebe Fred Kapondi (Mt. Elgon), Didmus Barasa (Kimilili), Khaoya Mulunda (Kanduyi), Barasa Wanjala (Kabuchai) na Mabongah Wekesa (Bumula).

Katika Kaunti ya Kakamega, chama cha Dkt Ruto kina wawaniaji wa ubunge katika maeneobunge 11 kati ya 12 kupambana na wale wa ANC.

Katika Kaunti ya Busia, chama cha UDA kina wawaniaji katika maeneobunge yote saba huku Bw Mudavadi akidhamini wagombeaji katika maeneobunge manne ya Nambale, Matayos, Butula na Budalangi. UDA pia kimesimamisha mwaniaji wa Mwanamke Mwakilishi, Susan Mang’eni.

Katika Trans Nzoia, UDA kina wawaniaji wa ubunge katika maeneobunge manne kati ya matano ambayo ni Saboti, Kiminini, Endebes na Cherangany. Naye Bw Wetang’ula amesimamisha wagombea wa Ford Kenya katika maeneobunge yote matano na mwaniaji wa ugavana, Chris Wamalwa.

KIAMBU NA LAIKIPIA

Katika Kaunti ya Kiambu ambayo ni ngome ya washirika wake, Bw Kabogo na Moses Kuria, chama cha UDA kimesimamisha wawaniaji wa ubunge katika maeneobunge yote 12. UDA pia kina mwaniaji wa ugavana, Kimani Wamatangi licha ya Bw Kuria na Bw Kabogo pia kuwania kiti hicho.

Katika Kaunti ya Laikipia, Bw Kiunjuri, ambaye ni mmoja wa vinara wa Kenya Kwanza, anamenyana vikali na mwaniaji wa UDA, Deddy Mohamed Amin katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Laikipia Mashariki.

AMASON KINGI

Nako Kaunti ya Kilifi, Dkt Ruto amesimamisha wawaniaji katika maeneobunge yote saba likiwemo eneobunge la Magarini nyumbani kwa kinara wa Pamoja African Alliance (PAA) Amason Kingi, ambaye ni mshirika wake mkuu. Chama cha PAA pia kina wawaniaji katika maeneobunge yote saba na mwaniaji wa ugavana, George Kithi anayemenyana na Aisha Jumwa wa UDA.

Katika Kaunti ya Machakos, UDA kimesimamisha wawaniaji katika maeneobunge yote, likiwemo Mwala ambako ni nyumbani kwa kiongozi wa chama cha Maendeleo Chapchap, Alfred Mutua.

Kwa jumla UDA kina wawaniaji ubunge 261 kote nchini huku ODM kikifuatia kwa wawaniaji 181 na Jubilee 178.

Vyama vya Jubilee na ODM, ambavyo vyote viko kwenye muungano wa Azimio, vimeachiana maeneo bunge katika baadhi ya kaunti kwa lengo la kuongeza idadi ya wabunge.

  • Tags

You can share this post!

Ugavana: Wazee wa Kaya wambariki Kithi

SHINA LA UHAI: Kisukari tishio kwa vijana pia

T L