• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Ruto amponda na kumpepeta Raila katika ngome yake

Ruto amponda na kumpepeta Raila katika ngome yake

Na CHARLES WASONGA

NAIBU RAIS William Ruto amemshambulia kiongozi wa ODM Raila Odinga katika ngome yake ya Luo Nyanza akidai handisheki kati ya Odinga na Rais Uhuru Kenyatta ilivuruga mipango ya maendeleo ya serikali ya Jubilee.

Dkt Ruto alisema mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) ulioongozwa na Bw Odinga alichangia serikali kukosa kutimiza miradi ya maendeleo ambayo ingefaidi eneo la Luo Nyanza.

Aliongeza kuwa eneo hilo limebaki nyuma kimaendeleo kutokana na siasa mbaya ambazo zimekuwa zikiendeshwa na viongozi waliokuwa wakishabikia marekebisho ya Katiba kupitia BBI.“Mpango wa BBI ulikuwa na ajenda fiche ya kuwapa mamlaka watu wachache.

Ulipoteza miaka minne ya serikali ya Jubilee ambayo ingetumiwa kutekeleza Agenda Nne Kuu za maendeleo,” akasema jana asubuhi kwenye mahojiano katika redio kadhaa zinazotangaza kwa Dholuo. Mahojiano hayo yaliendeshwa katika mkahawa wa Ciala Resort mjini Kisumu.

Dkt Ruto alikariri kuwa lengo kuu la marekebisho ya Katiba kupitia BBI lilikuwa ni kurejesha utawala wa Rais mwenye mamlaka ya kiimla.“Mengi ya mapendekezo yaliyopendekezwa katika BBI yangeweza kutekelezwa bila Katiba kufanyiwa marekebisho kupitia kura ya maamuzi,” akaeleza huku akiwarai wakazi wa eneo hilo kuunga agenda yake ya maendeleo ya “Bottom Up”.

Dkt Ruto ambaye alianza ziara yake eneo hilo Jumanne, pia alimshambulia Bw Odinga kwa kuongoza chama ambacho hakina sura ya kitaifa. Alisema chama cha ODM hakina ajenda maalum ya maendeleo licha ya kubuniwa miaka 15 iliyopita.

“Hauwezi kuendesha chama cha kikabila kwa miaka 15 huku ukidai ni cha kitaifa. Mbona unadai kuwa unataka kuwania urais ilhali chama chako kimejengwa kwa misingi ya kikabila?” Dkt Ruto akauliza.

Naibu Rais alikariri kuwa chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) ndicho chama cha kipekee chenye sura ya kitaifa nchini kwa sababu sera zake zinalenga rais wa matabaka yote.“UDA chenye alama ya wilbaro ni chama cha kitaifa ambacho kimejitolea kuwahudumia watu wote matajiri na masikini.

Nashangaa ni kwa nini wale tunaoshindana nao hukejeli alama yetu ya wilbaro ilhali mimi sijawahi kukosa alama zao za machungwa, simba na vitu vinginevyo,” Dkt Ruto akasema.Dkt Ruto aliahidi kuwa akishinda urais katika uchaguzi mkuu ujao, serikali yake itotoa kipaumbele kwa mpango wa ufufuzi wa serikali ya kilimo na uvuvi katika eneo zima la Nyanza.

Baada ya mahojiano hayo mkutano wa Dkt Ruto katika eneo la Kondele ulikumbwa na vurugu baada ya vijana kuanza kurusha mawe wakiimba nyimbo za kuisifu ODM na Bw Odinga.

You can share this post!

Kananu kurithi kiti dhaifu cha ugavana jijini

Kenya yaipiga breki tena Uganda Cranes G mechi ya kufuzu...

T L