• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Kenya yaipiga breki tena Uganda Cranes G mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2022

Kenya yaipiga breki tena Uganda Cranes G mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2022

Na CECIL ODONGO

TIMU ya taifa Harambee Stars jana ilipiga breki juhudi za Uganda kuingia raundi ya mwisho ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022, baada ya kulazimisha sare ya 1-1 katika uga wa St Mary’s Kitende jijini Kampala.

Nahodha na mvamizi wa Stars Michael Olunga alifunga bao la Kenya kupitia mpira wa kichwa, baada ya kumegewa pasi nzuri kutoka katikati mwa uwanja na Kenneth Muguna aliyechanja vyema mpira wa ikabu kunako dakika ya 62.

Uganda ilisawazisha dakika ya 88 kupitia Fahad Bayo aliyejaza mpira wavuni kirahisi kutokana na masihara ya mnyakaji wa Harambee Stars Brian Bwire ambaye anachezea timu ya Tusker.Goli hilo litazua maswali tele ikizingatiwa kuwa Bwire alikuwa amezuia mpira vizuri ila akachelewa kuuondoa mbele ya goli naye Bayo ambaye alikuwa karibu akampokonya kirahisi na kuujaza wavuni kusawazishia Cranes.

Hii likuwa sare ya tatu kwa vijana wa kocha Engin Firat katika kundi E tangu michuano hiyo ianze, ingawa Kenya hata ingeshinda mechi hiyo bado haingefuzu raundi ya mwisho.Pia sare hiyo inamaanisha kuwa Kenya haijapiga Uganda ugenini tangu 2004 ambapo ililemea Cranes nyumbani kwao 2-1 katika mechi ya kirafiki.

Kutokana na sare hiyo, Kenya sasa imejizolea alama tatu katika kundi hilo.Ilipiga sare tasa dhidi ya Uganda mnamo Septemba 2, ikapata 1-1 dhidi ya Rwanda mnamo Septemba 5. Hata hivyo, ililemewa 5-1 na 1-0 na Mali mnamo Oktoba 7 na Oktoba 10.

Uganda ililazimika kutegemea Rwanda iipige Mali nyumbani, katika mechi ambayo ilichezwa baadaye jioni, ili kuwa na matumaini ya kupigana katika mechi ya mwisho dhidi ya Mali.Sare hiyo na Kenya iliacha Uganda ikiwa na alama tisa, ambapo Mali ingetwaa tiketi ya pekee ya kundi hilo iwapo ingepata ushindi dhidi ya Rwanda jana jioni.

Sare hiyo iliibua kumbukumbu za 2012 ambapo Stars ilikazia Cranes kwenye mechi iliyoishia sare tasa, matokeo yaliyozuia Uganda kufuzu AFCON, baada ya kuwa nje kwenye baridi kwa muda wa zaidi ya miaka 20.

Mkufunzi wa Cranes Milutin Sredojevic alisema Kenya iliwapa upinzani mkali na vijana wake ndio walikosa kutumia vyema nafasi walizopata katika mechi.Huku serikali ikichukua usimamizi wa soka nchini, hatima ya kocha wa Stars Firat haijulikani ikizingatiwa Shirikisho la Soka Nchini (FKF), ambalo lilimpa mkataba wa miezi miwili, limeondolewa uongozini na kamati ya muda kubuniwa.

Rais wa FKF Nick Mwendwa mnamo Septemba alisema kuwa kocha huyo Mturuki alifaa kuongoza Kenya katika mechi nne zilizosalia za kufuzu Kombe la Dunia.

You can share this post!

Ruto amponda na kumpepeta Raila katika ngome yake

Sasa Man-United yakanusha madai kumhusu Ronaldo

T L