• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 2:11 PM
Ruto aonekana kuwa kigeugeu akiwa ng’ambo

Ruto aonekana kuwa kigeugeu akiwa ng’ambo

NA LEONARD ONYANGO

HOTUBA za Naibu wa Rais William Ruto ughaibuni zimezidi kuwakanganya wafuasi wake, huku wadadisi wakisema kuwa zimempa taswira ya kiongozi kigeugeu.

Naibu Rais Ruto ametumia ziara yake katika mataifa ya Amerika na Uingereza, kutoa madai mbalimbali dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta, serikali ya Jubilee, baraza la mawaziri na hata kudai kuwa kuna mpango wa kuiba kura za urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Dkt Ruto alipokuwa anahutubu katika ukumbi wa Chatham House nchini Uingereza, alikiri kuwa asilimia 30 ya vipengele ndani ya Katiba vinahitaji kufanyiwa marekebisho.

Wakati huo, Naibu wa Rais alipendekeza Katiba ifanyiwe marekebisho ili kubuni wadhifa wa kiongozi wa upinzani ili aweze kukosoa serikali.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba mwaniaji wa urais anayeibuka nafasi ya pili baada ya kupata mamilioni ya kura anatupwa nje na kuwa mgeni,” alisema Dkt Ruto.

Ni katika hotuba hiyo ambapo Dkt Ruto alishikilia kuwa wanasiasa wanaohisi kushindwa ndio hulaumu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Watu ambao hawashindi uchaguzi ndio hupendelea kulaumu IEBC. Shida tuliyo nayo si usimamizi wa uchaguzi bali shida kubwa ni viongozi ambao hawataki kukubali matokeo. Shida ya Kenya ni kwamba tuna watu ambao hawaamini demokrasia. Wanaingia kwenye siasa wakiamini kwamba watashinda,” akasema Dkt Ruto.

Lakini katika hotuba yake nchini Amerika wiki iliyopita na jumba la Chatham Jumatatu, Dkt Ruto alipuuzilia mbali jaribio la Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, kutaka kurekebisha Katiba kupitia Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Mswada wa BBI ambao sasa uko katika Mahakama ya Juu baada ya kutupwa na Mahakama Kuu na Rufaa, unapendekeza kubuniwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani atakayetengewa serikali na Jubilee.

Dkt Ruto Jumatatu, aliambia Wakenya wanaoishi nchini Uingereza kuwa, atatengeneza kituo chake mbadala cha kujumulisha matokeo.

Kulingana na wandani wa Naibu wa Rais, serikali imeanza kuingilia shughuli za IEBC kwa lengo la kuiba kura.

Kulingana na wanasiasa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), kituo cha kujumlisha matokeo kimekamilika na maafisa watakaohudumu hapo wameanza kupewa mafunzo.

Mnamo Machi 2017, Dkt Ruto alishutumu vikali mpango wa muungano wa Nasa ulioongozwa na Bw Odinga kwa kutaka kuweka kituo mbadala cha kujumlisha matokeo huku akisema kuwa hatua hiyo ilikiuka Katiba.

Naibu wa Rais aliyekuwa akizungumza katika eneo la Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, alisema jukumu la kujumlisha matokeo lilikuwa la IEBC.

“Sasa ni wazi kwamba viongozi wa upinzani wameishiwa na mbinu za kusaka kura na sasa wanataka kujijumlishia matokeo ili wajitangaze washindi,” alisema Naibu wa Rais.

Siku nne kabla ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017, serikali ilifurusha kwa nguvu wataalamu wa kigeni walioletwa humu nchini na Bw Odinga kusimamia kituo mbadala cha kujumulisha matokeo cha Nasa.

Serikali ilidai kuwa wataalamu hao wanne – John Aristotle Philips (Mwamerika), Andreas Katsouris (Mkanada) na raia wawili wa Ghana – hawakuwa na kibali cha kufanya kazi humu nchini.

Katika hotuba yake ya Jumatatu, Dkt Ruto alilaumu baraza la mawaziri kwa kusababisha serikali ya Jubilee kufeli.Naibu wa Rais alisema kuwa Rais Kenyatta alimpokonya majukumu yake mnamo 2019 na kuyakabidhi kwa waziri wa Usalama Fred Matiang’i.

“Watu waliokabidhiwa majukumu na Rais Kenyatta walimwangusha kwani walishindwa kufanya kazi na kusababisha kuporomoka kwa miradi ya Ajenda Kuu Nne (ustawishaji wa viwanda, kuboresha huduma za afya, kuongeza uzalishaji wa chakula na kutoka makazi ya bei nafuu),” alisema Naibu wa Rais.

Katika mikutano yake ya kisiasa humu nchini, Dkt Ruto amekuwa akilaumu Bw Odinga kwa kusababisha serikali ya Jubilee kufeli.

Amekuwa akisema handisheki baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga mnamo 2018 ilisababisha serikali kushindwa kutekeleza miradi ya Ajenda Kuu Nne.

You can share this post!

Bayern waingia robo-fainali za UEFA baada ya kurarua RB...

Aliyetoweka kwake 1973 apatikana Lamu

T L