• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Ruto aonywa asifuate nyayo za Raila kisiasa

Ruto aonywa asifuate nyayo za Raila kisiasa

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto ameonywa kuwa atashindwa kuafikia malengo yake ya kushinda urais 2022, ikiwa ataendelea kuiga mbinu za kisiasa zilizotumiwa na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga katika miaka iliyopita.

Hapo jana, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee (JP), Bw David Murathe, alisema Bw Odinga alifanya makosa kwa mfano alipoanza ukaidi ndani ya serikali alipokuwa Waziri Mkuu, na huenda Dkt Ruto akarudia makosa hayo hayo.

“Kosa alilofanya Bw Odinga ni kuanza kumsumbua Mzee Kibaki kuhusu mamlaka. Alidai kutengwa ama kutoshirikishwa kwenye maamuzi fulani ya serikali. Alipoteza subira. Leo angekuwa rais, kwani ni wazi Mzee Kibaki angemuunga mkono baada yake kung’atuka 2013,” akasema Bw Murathe.

Bw Odinga alikuwa Waziri Mkuu chini ya serikali ya mseto iliyoongozwa na aliyekuwa rais Mwai Kibaki baada ya ghasia za uchaguzi wa 2007.

Wadadisi wa siasa wanasema kuwa Dkt Ruto ni ‘mwanafunzi wa kisiasa’ wa Bw Odinga ndiposa mbinu anazotumia kutafuta umaarufu miongoni mwa Wakenya zinakaribiana na zile za Bw Odinga.Kwa mfano, wanasema msingi wa siasa za Bw Odinga unaelezwa kuwa uasi dhidi ya utawala uliopo tangu alipojitosa siasani katika miaka ya tisini.

Alipokuwa waziri mkuu katika serikali ya Kibaki, wakati mwingine alilalamika mawaziri wa chama cha PNU hawakuwa “wakimtii” au hakuwa akishirikishwa kwenye baadhi ya maamuzi ya serikali.

Wadadisi wanasema kuwa kwa kudai kutengwa, kuonewa na baadhi ya majukumu yake kupewa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Dkt Ruto anafuata nyayo hizo za Bw Odinga.

“Hawa ni wanasiasa wawili ambao wamekuwa wakitangamana kwa muda mrefu. Dkt Ruto amekaidi maagizo ya Rais Kenyatta kutofanya kampeni za 2022. Analenga kubuni dhana ya ‘mtoto aliyetengwa na mzazi wake’ ili kupata huruma kutoka kwa wafuasi wake,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Bw Odinga pia amekuwa akidai alisalitiwa na Mzee Kibaki, washirika wake na eneo la Mlima Kenya, licha ya kumuunga mkono kwenye uchaguzi wa 2002, kupitia kauli ya ‘Kibaki Tosha.’

Vivyo hivyo, wadadisi wanasema mwelekeo huo ndio anaofuata Dkt Ruto.’Dkt Ruto analenga kujisawiri kama mwanasiasa mzalendo, mwaminifu na anayeweza kusimama na rafikiye hadi anapopitia katika nyakati ngumu. Kama Bw Odinga, ni mbinu anayotumia, hasa kuwavutia wapigakura,” asema Prof Macharia Munene.

Hata hivyo, wadadisi wanasema itakuwa vigumu kwa Dkt Ruto kuendeleza mbinu hizo, ikiwa ataendelea kuwa serikalini.“Tayari, ashabuni dhana ya kiongozi wa upinzani, ingawa hataki kukubali hivyo. Imefikia wakati atathmini mwelekeo wake kisiasa,” asema Bw Mark Bichachi, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana na wadadisi, wafuasi wengi wa Bw Odinga humwona kama mkombozi anayewapa imani hata wakati nyakati zinakuwa ngumu.

Wengi bado wanaamini atawafikisha ‘Kanani’.Vivyo hivyo, Dkt Ruto anajaribu kujionyesha ndiye mkombozi hasa kwa vijana na walalahoi kupitia vuguvugu lake la ‘hasla’.

You can share this post!

Udikteta ulivyolemaza vita dhidi ya corona Tanzania

Dortmund wapiga Gladbach na kutinga nusu-fainali za German...