• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 4:39 PM
Ruto asema hana shida na maafisa wa IEBC

Ruto asema hana shida na maafisa wa IEBC

NA CHARLES WASONGA

MGOMBEA urais wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) William Ruto amesema kuwa hana malalamishi kuhusu namna Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliajiri maafisa watakaosimamia uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Akiongea Jumatano katika mkutano kati ya wakuu wa tume hiyo na wagombea urais wanne, Dkt Ruto alisema kuwa mradi maafisa hao wamehitimu na wametueliwa kwa kufuatia taratibu za kisheria, atakubali kushirikiana nao.

“Bw Mwenyekiti nimewahi kusema kuwa hata ikiwa kakake mpinzani wangu ndiye atakuwa mwenyekiti wa IEBC sitakuwa na shida mradi awe ameteuliwa kwa njia ya haki,” akasema Dkt Ruto.

Akiongea katika ibada ya Jumapili katika kanisa moja la Anglikana mjini Embu mnamo Desemba 19, 2020 Dkt Ruto alielezea imani kwamba uchaguzi mkuu ungeitishwa mwaka huo, angembwaga Bw Odinga “hata kama ndugu yake, Oburu Oginga, ndiye atateuliwa mwenyekiti wa IEBC.”

Dkt Ruto alitoa kauli ya Jumatano baada ya ajenti mkuu wa Bw Odinga katika uchaguzi wa urais Bw Saitabao Ole Kanchory kuelezea kutoridhishwa kwake na jinsi IEBC ilivyoteua wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi za kaunti.

Kulingana na ajenti huyo, wasimamizi wanane (8) kati ya 47 wanatoka jamii moja, hali ambayo alisema haionyeshi usawa.

“Iweje kwamba IEBC iliteua watu wanane kutoka jamii moja ambako mgombeaji mmoja wa urais anatoka, kuwa wasimamizi wa uchaguzi katika kaunti ilhali Kenya ni taifa lenye karibu makabila 50?” akauliza Bw Kanchory.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wagombeaji wengine; David Waihiga Mwaure wa chama cha Agano na Profesa George Wajackoyah wa chama cha Roots.

  • Tags

You can share this post!

Mwaniaji ugavana Kiambu aitaka serikali ihakikishe Wakenya...

Fernandinho arejea Brazil kuchezea Athletico Paranaense...

T L