• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Ruto awapongeza magavana wanawake walioapishwa

Ruto awapongeza magavana wanawake walioapishwa

NA WINNIE ONYANDO

RAIS Mteule, William Ruto amewapongeza wanawake walioapishwa Alhamisi kuwa magavana katika kaunti mbalimbali nchini.

Akizungumza katika hafla ya kuapishwa kwa Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja na Naibu wake, James Njoroge Muchiri, Dkt Ruto alisema kuwa kuchaguliwa kwa akina mama katika nyadhifa mbalimbali ni mwamko mpya kisiasa nchini.

“Nawapongeza wanawake wote walioapishwa leo. Hiyo ni ishara tosha kuwa hata akina mama wana uwezo wa kuongoza,” akasema Dkt Ruto.

Rais Mteule William Ruto (kati) akiwa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja (wa pili kushoto) na Naibu wake James Njoroge Muchiri (kushoto). PICHA | HISANI

Amempongeza aliyekuwa Mwakilishi wa jinsia ya Kike Homa Bay Gladys Wanga ambaye kwa sasa ni Gavana wa Homa Bay, Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru, Gavana wa Embu Cecily Mbarire, Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti, Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, Gavana wa Kwale Fatuma Achani na Gavana wa Nakuru Susan Kihika kwa kuonyesha ujasiri katika kampeni.

Kadhalika, Dkt Ruto amesema kuwa serikali itakayoundwa itashirikiana na gavana Sakaja kukarabati na kusafisha majitaka na kuboresha mito iliyoko Nairobi.

Kwa upande wake, gavana Sakaja ameahidi kushirikiana na Idara ya Kusimamia Jiji (NMS) ili kuendeleza miradi ya maendeleo yaliyoanzishwa na mwenyekiti wa idara hiyo, Mohamed Badi.

“Niko tayari kushirikiana na viongozi wote ili kuboresha utoaji huduma Nairobi,” akasema Bw Sakaja.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume seli kujaribu kujiua sababu ya deni

Magavana wapya kurithi dhambi za watangulizi

T L