• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 2:31 PM
Afueni kwa wasafiri baina ya Lamu na Garsen mawe yakipangwa Gamba kuunganisha barabara iliyokatwa na mafuriko

Afueni kwa wasafiri baina ya Lamu na Garsen mawe yakipangwa Gamba kuunganisha barabara iliyokatwa na mafuriko

NA KALUME KAZUNGU

NI afueni kwa mamia ya wasafiri baina ya Lamu na Garsen baada ya mawe kupangwa kufunika eneo la Gamba lililosombwa na mafuriko yaliyobeba mchanga uliokuwa ni sehemu muhimu ya barabara majuma mawili yaliyopita.

Eneo hilo la barabara lenye urefu wa karibu nusu ya kilomita lilikuwa limegeuka mto wenye maji mengi badala ya barabara,hali ambayo ilikuwa imelemaza kabisa usafiri kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Kwa kipindi cha majuma mawili sasa, wasafiri waliokuwa wakitoka Lamu kuelekea Mombasa na wale wa Mombasa kuingia Lamu hawangeweza kuvuka eneo la Gamba.

Aliyekuwa na azma ya kusafiri kwenye barabara hiyo alilazimika kusafiri kwa magari na kisha kushuka na kutumia madau madogo ambayo yalikuwa yakitumika kuwavukisha.
Wasafiri hao kisha walitakiwa kuunganisha upya na kuendeleza safari zao Kwa magari mengine ambayo yalikuwa yakisubiri upande mwingine.

Hali hiyo ilikuwa imeathiri pakubwa uchukuzi na hata kupelekea miji mikuu kama vile Witu, Mpeketoni,Hindi,Mokowe na kisiwa cha Lamu kuanza kushuhudia uhaba wa bidhaa muhimu,ikiwemo chakula,mafuta ya petroli na dizeli kutokana na usafiri wa barabarani kukatizwa.

Ni kutokana na hali hiyo ambayo iliisukuma serikali kuanzisha harakati za kurejelewa kwa usafiri wa barabarani Lamu kupitia ukarabati wa sehemu hiyo ya Gamba iliyoharibiwa na mafuriko.

Kwa karibu kipindi cha juma moja sasa serikali kupitia kwa Mamlaka ya Ujenzi na Usimamizi wa Barabara kuu nchini (KeNHA), imekuwa ikiendeleza ukarabati,ikiwemo malori yaliyojazwa mchanga, mawe na kokoto yakifika Gamba kumwaga vifaa hivyo vya ujenzj kwa minajili ya kufunika shimo la barabara.

Ni shughuli ambayo ilitekelezwa kwa mwendo wa konokono kwani matingatinga yaliyokuwa yakitumiwa kutandaza mawe hayo yalipata taabu kutokana na hali mbaya iliyokuwepo Gamba.

Kufikia Jumatano aidha, mwanakandarasi wa mradi huo wa ukarabati tayari alikuwa amefaulu kuunganisha sehemu hiyo ya barabara iliyokatwa,hivyo kupisha wasafiri,japo wachache wa miguu wakianza kutumia sehemu hiyo kuvuka pande nyingine.

Bw Emmanuel Wanyoike, mmoja wa watumiaji wa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, alishukuru serikali kwa juhudi zake katika kuhakikisha usafiri wa barabara unarejelewa.

“Tumefurahia sana kuona bidii za serikali yetu tukufu ikikarabati eneo hili la Gamba lililokatwa na mafuriko. Japo ukarabati umechukua muda kabla uanze lakini twaona mwanga wa matumaini mbele. Najua kuna zile familia zinazomiliki magari ya kibinafsi ambazo tayari zilikuwa zimekata tamaa ya kufika Lamu au kutoka eneo hili kwenda kujumuika na ndugu,jamaa na marafiki kusherehekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya. Nataka kuwaambia nipo hapa na tayari wenye miguu wameanza kuvuka kwani eneo limeunganishwa. Magari pia yataanza kupita hapa si kitambo,” akasema Bw Wanyoike.

Naye Bw Abdulrahman Yusuf, mkazi wa Lamu, alishukuru kuona kwamba usafiri wa barabarani unarejelewa.

Bw Yusuf alikumbuka mateso ambayo wakazi wa Lamu wamepitia hasa tangu usafiri wa barabarani kusitishwa kutokana na athari za mafuriko.

“Kipindi cha majuma mawili yaliyopita kimekuwa cha dhiki si haba. Ila twashukuru kwamba angalau serikali imeonyesha kutujali kwa kukarabati eneo hili la Gamba lilillsombwa na mafuriko. Mimi ni mmoja wa wale waliovuka Gamba kwa miguu mnamo Jumatano baada ya barabara kuunganisha,” akasema Bw Yusuf.

Wamiliki wa magari ya usafiri wa umma ni miongoni mwa wanaofurahia kukarabatiwa na kuunganishwa kwa barabara ya Lamu-Witu-Garsen.

Bw Said Swaleh,mmoja wa makondakta wa mabasi ya usafiri wa umma yanayohudumia barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, alitaja kurejelewa kwa usafiri barabarani kuwa mwanzo mpya kwao.

“Hata sisi watoaji huduma za mabasi ya usafiri wa umma tumeumia. Biashara ilikosekana kipindi chote cha majuma mawili ya mafuriko. Kukarabatiwa kwa Gamba ni kumaanisha biashara ya usafiri imerejea sasa. Twashukuru angalau familia zetu zitapata riziki,” akasema Bw Swaleh.

Barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen ndicho kiunganishi cha pekee cha Lamu na maeneo mengine ya Kenya, hasa kwa wale wanaotumia usafiri wa nchi kavu.

  • Tags

You can share this post!

Sabina Chege: Raila angeshinda urais mwaka 2022 ikiwa...

Kang’ata afafanua kuhusu waraka uliotangaza...

T L