• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Safari ya chama kimoja yaanza

Safari ya chama kimoja yaanza

NA BENSON MATHEKA

SAFARI ya Rais William Ruto kuunganisha vyama tanzu vya muungano tawala wa Kenya Kwanza kuwa chama kimoja kikubwa imeanza baada ya vyama sita kukubali kumezwa na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA).

Hatua hii inajiri huku Rais Ruto akiwinda wabunge wa vyama vya upinzani kwa kile anachotaja kama “kushirikiana na viongozi wote waliochaguliwa bila kujali mirengo ya kisiasa” na kunyemelea viongozi wa zamani wenye ushawishi kutoka ngome za upinzani.

Mwezi Februari, kiongozi wa nchi alikutana na wabunge 9 wa chama cha ODM kinachoongozwa na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa mwaka jana Raila Odinga, na wabunge 30 wa Jubilee ambao walijaribu kufanya mapinduzi katika chama hicho kinachoongozwa na Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta.

Jana Jumanne, Katibu Mkuu wa chama cha UDA, Cleophas Malala, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhimiza vyama tanzu vya Kenya Kenya kuvunjiliwa mbali aliongoza vyama sita kati ya 17 vinavyounda muungano huo tawala kumezwa na chama cha Rais Ruto.

Vyama hivyo ni Umoja na Maendeleo kinachoongozwa na aliyekuwa gavana wa Embu Martin Wambora, Farmers Party of Kenya chini ya uongozi wa aliyekuwa katibu wa wizara Irungu Nyakera, Economic Freedom Party kinachoongozwa na Isaac Hassan Abey na Chama cha Mashinani kinachoongozwa na Mohamed Gulei.

Vyama vingine vilivyomezwa na UDA ni National Agenda Party kinachoongozwa na Alfayo Agufana na Chama Cha Kazi kinachoongozwa na Bw James Kimani.

Vyama hivyo vimefuata nyayo za Chama cha Kazi kilichoongozwa na Waziri wa Biashara na Viwanda Moses Kuria kilichomezwa na UDA mwaka 2022.

Hatua ya vyama hivyo inaonekana kuwa mwanzo wa mwelekeo ambao vyama vingine tanzu vya Kenya Kwanza vitachukua ingawa Bw Malala alisema vina haki ya kuchagua kumezwa au la.

“Vyama vya kisiasa viko na haki ya kuchagua vinavyotaka. Baadhi vitaamua kubaki kuwa huru na bado tutashirikiana navyo na baadhi vitakubali kujiunga na UDA, tunawakaribisha ( viongozi) na tutahakikisha wamekuwa wanachama na tutawafanya maafisa na wanachama wa chama chetu. Tumewapatia idhini ya kushiriki katika uchaguzi wa mashinani wa UDA,” Bw Malala alisema.

Seneta huyo wa zamani wa Kakamega ameonekana kutimiza ahadi yake alipoteuliwa Katibu Mkuu wa UDA wiki tatu zilizopita ya kuhakikisha jukumu lake la kwanza ni kuunganisha vyama tanzu vya Kenya Kwanza nyuma ya Rais Ruto.

Msimamo wake ambao wadadisi wanasema una Baraka za Rais Ruto ulipingwa na chama cha Amani National Congress (ANC) kilichoanzishwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na Maendeleo Chap Chap cha Waziri wa Mashauri ya Kigeni Dkt Alfred Mutua.

Kumezwa kwa vyama hivyo sita jana Jumanne, kunaonekana kuwa presha kwa vyama hivi vitatu na vingine vya Kenya Kwanza kukubali kuvunjwa ili UDA iwe na nguvu zaidi ndani na nje ya Bunge.

“Tumeketi na vyama vinane katika UDA na tumekubaliana kuwa tunahitaji kuwa chini ya mwavuli mmoja ambao utasaidia rais wetu kuzingatia ajenda yake kwa kutumia mwavuli huo tunapojiandaa kwa siasa za 2027,” Bw Malala alisema.

Mdadisi wa siasa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watumiaji Bidhaa Kenya Cofek) Stephen Mutoro alitaja hatua ya kumezwa kwa vyama hivyo na UDA kama ushindi mkubwa kwa Rais Ruto.

“Dalili za mwanasiasa hodari, mwerevu Afrika na anayejua kucheza karata zake. Rais William Ruto amepata ushindi mkubwa huku vyama sita vya muungano wa Kenya Kwanza vikimezwa na chama cha UDA,” akasema Bw Mutoro.


  • Tags

You can share this post!

AFYA: Vidokezo vya jinsi ya kupunguza ‘uzito wa...

Chuo chatimua wanafunzi wenye vyeti feki vya KCSE

T L