• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Shinikizo kwa Ruto, Raila wazungumze

Shinikizo kwa Ruto, Raila wazungumze

CHARLES WASONGA Na JESSE CHENGE

WITO wa kumtaka Rais William Ruto kufanya mazungumzo na Upinzani umeshika kasi siku moja baada ya kinara wa Azimio Raila Odinga kuongoza maandamano yaliyokwamisha shughuli katika maeneo mbalimbali nchini, Jumatatu.

Hii ni licha ya Bw Odinga kutangaza kuwa, kuanzia wiki ijayo maandamano hayo yatafanya Jumatatu na Alhamisi kuishinikiza serikali ipunguze gharama ya maisha, miongoni mwa matakwa mengine.

Jana Jumanne, viongozi wa kidini na baadhi ya wanasiasa waliwataka Rais Ruto na Bw Odinga kulegeza misimamo yao mikali na kufanya mazungumzo kurejesha amani nchini.

Viongozi hao wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo na dini ya Kiislamu kutoka Bungoma, Meru na Malindi walitaka wawili hao kuweka masilahi ya nchi mbele kwa kuzima uhasama wa kisiasa ambao umegubika taifa hili.

Naye Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja aliwataka Rais Ruto na Bw Odinga kuelewana ili kukomesha maandamano hayo aliyosema yalichangia serikali yake kupoteza mapato ya takribani Sh40 milioni.

Kwa upande wake, muungano wa viongozi wa madhehebu mbalimbali kaunti ya Bungoma walisema maandamano hayo yaliathiri vibaya biashara, uchukuzi na masomo kote nchini.

“Kiongozi wa Azimio Raila Odinga na Rais William Ruto kama viongozi wenye ufuasi mkubwa nchini Kenya wanafaa kukumbatia mazungumzo kwa kuwa hiyo ndio njia ya kipekee ya kukomesha uharibifu wa mali ulioshuhudiwa katika maandamano ya jana (Jumatatu),” Mwenyekiti wa muungano huo Calistus Barasa akasema kwenye kikao na wanahabari mjini Bungoma.

Nao viongozi wa kidini kutoka eneo la Igembe, kaunti ya Meru waliwaomba Rais Ruto na Bw Odinga kupatana ili kuokoa taifa hili kutoka kwa lindi la machafuko.

Wakiongea katika hafla ya mapasta na wake zao katika eneo la Antubochiu, Igembe Kusini, mwenyekiti wa Shirikisho la Mapasta eneo la Igembe (Igembe Pastors’ Network-IPN), Sammy Mwithalie alisema maandamano yatahujumu juhudi za serikali za kufufua uchumi.

Nayo makanisa wanachama wa Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) kaunti ndogo ya Malindi yalitoa wito kwa Wakristo kuendelea kuwaombea Rais Ruto na Bw Odinga ili wakubali miito ya kuwataka wazungumze.

“Kama Wakristo, tunafaa kufanya maombi kila mara ili amani irejee nchini. Vile vile, tuwakumbuke Rais Ruto na Bw Odinga katika maombi ili waweze kukomesha maandamano haya. Hakuna maandamano yanayoweza kufanyika kwa amani kwa sababu wahalifu wataingilia na kupora mali,” akasema Katibu wa Kanisa la PEFA, Malindi Christopher Ziro.

Wakati huo huo, Baraza la Maimam na Wahubiri Nchini Kenya (CIPK) limetoa wito kwa viongozi wa kisiasa nchini kuvumiliana na kuhubiri amani wakati huu ambapo mfungo wa Mwezi Mtufuku wa Ramadhani unakaribia kuanza.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa, Katibu Mratibu wa CIPK, Sheikh Mohamed Khalifa alimtaka Bw Odinga kufutilia mbali maandamano “kama heshima kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani”.

Lakini akiongea katika Ikulu ya Nairobi Jumatatu, Rais Ruto alishikilia kuwa serikali yake haitavumilia vitendo vya ukiukaji sheria vinavyoendelezwa na Azimio. Wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa, wabunge na maseneta wa muungano huo tawala walishikilia kuwa Rais Ruto hawezi kufanya mazungumzo na Bw Odinga.

“Rais Ruto hana wakati wa kupoteza kuzungumza na mtu ambaye nia yake ni kuhujumu serikali yake kupitia maandamano na uharibifu wa mali na kusababisha maafa. Huyu ni mtu ambaye anapaswa kukamatwa na kushtakiwa kwa sababu yuko chini ya sheria,” mbunge huyo wa Kikuyu aliambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Lakini kwa upande wao, viongozi wa Azimio, wakiongozwa na kiongozi wa wachache katika Seneti Stewart Madzayo na mwenzake wa Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi walishikilia kuwa maandamano hayo yataendelea.

  • Tags

You can share this post!

Vitisho vya wazazi kwa walimu wakuu huchochea wizi wa...

Gavana: Toeni fungu la 10

T L