• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Sitajiuzulu kama Spika, Muturi asema

Sitajiuzulu kama Spika, Muturi asema

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amepuuzilia mbali miito ya kumtaka ajiuzulu mnamo Februari, 2022 sawa na watumishi wa umma wanaopania kuwania viti vya kisiasa katika uchaguzi ujao.

Kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen, Bw Muturi alisema kuwa ataendelea kushikilia wadhifa wake hadi siku ya uchaguzi mkuu, Agosti 9, mwaka huo, sawa na wabunge. Ametangaza azma ya kuwania urais katika uchaguzi kwa tiketi ya chama cha kisiasa ambacho hajakitaja rasmi.

Kulingana na Spika Muturi kikatiba yeye sio mtumishi wa umma bali ni mbunge japo huchaguliwa na wabunge sio raia.

“Nani anasema mimi ni mtumishi wa umma? Kulingana na Katiba Spika ni mtu ambaye amehitimu kuwa mbunge na baada ya kuchaguliwa, kula viapo viwili; moja kama Spika na nyingine kama mbunge,” akaeleza.

“Kando na madiwani ambao wanazuiwa na Katiba kuwania nyadhifa zingine kabla ya wao kujiuzulu, wabunge hawahitajiki kujiuzulu kuwania nyadhifa zingine kama za ugavana au useneta,” Bw Muturi akasema.

Spika huyo pia alitoa mfano wa Rais ambaye hahitajiki kujiuzulu wakati ambapo anatetea kiti hicho uchaguzini baada ya kuhudumu kwa muhula wa kwanza.

Bw Muturi pia alikariri kuwa ndoto yake ya kuwania urais 2022 hautaathiri kwa vyovyote utendakazi wake kama Spika wa Bunge la Kitaifa na mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

“Haitaingilia kwa njia yoyote jinsi ambavyo nitaongoza shughuli za bunge kama Spika. Wajibu wangu ndani ya bunge ni kuhakikisha kuwa sheria na kanuni za bunge zitafutwa sawa na Katiba ya nchi. Siwezi kutumia kiti hicho kuomba kura za urais”.

“Lakini nikitoka nje bila shaka nitakuwa huru kuuza sera zangu na kusaka uungwaji mkono kama mgombeaji urais,” akafafanua.

Bw Muturi vile vile, alisema wakati kama huu hataegemea chama chochote cha kisiasa au muungano wowote bali atajitahidi kuuza sera zake kwa raia.

“Wakati ukifika nitatangaza chama ambacho nitakitumia kuwania urais. Chama hicho kitakuwa ni kila kinapigania haki ya kijamii. Lakini siwezi kuanza kuendesha mazungumzo kuhusu uundaji wa miungano kwa sababu hatua kama hiyo itanifanya kuonekana kiongozi mnyonge,” akaeleza.

Baadhi ya wanasiasa wanaopinga ndoto za Bw Muturi za kuwania urais na kutawazwa kwake kama Msemaji wa Mlima Kenya wamekuwa wakimshinikiza ajiuzulu wadhifa anaoshikilia sasa kama Spika wa Bunge la Kitaifa.

You can share this post!

Tutaheshimu uamuzi wa mahakama ya rufaa kuhusu BBI –...

Ajizolea umaarufu kwa kutunga nyimbo za kisiasa