• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Sitastaafu na siendi kokote, Raila asema

Sitastaafu na siendi kokote, Raila asema

MACHARIA GAITHO Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga sasa ametangaza bayana kwamba hatastaafu siasani na kwamba atawania uchaguzi mkuu wa 2027.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 78, anasema hawezi kuwatelekeza wananchi kwa kustaafu siasa akiapa kupamba na utawala wa Rais William aliutaja kama anaopania kurejesha Kenya katika enzi ya utawala wa kidikteta wa Hayati Daniel Moi.

Japo wakati wa uchaguzi mkuu wa 2027 Bw Odinga atakuwa na umri wa miaka 82, mwanasiasa huyo anashikilia kuwa “bado nina kazi ya kufanya”.

Katika mazingira hayo, anasema, hawezi kuwatelekeza wananchi kwa kustaafu siasa.Mnamo Januari 8, mwaka huu aliadhimisha miaka 78 tangu kuzaliwa kwake.

Kwenye mahojiano ya kipekee na jarida la Darubini ya Wiki afisini mwake Jumba la Capitol Hill, Nairobi juzi, kiongozi huyo wa upinzani alielezea imani kwamba Azimio itasalia thabiti wakati wa uchaguzi mkuu wa 2027.

“Bado niko na nguvu licha ya umri wangu mkubwa na niko tayari kuendelea. Lakini niko tayari kuwaacha wengine. Nina na watu tunaoshirikiana nao na ambao wamekuwa imara kama vile Kalonzo Musyoka,” akasema.

Akaongeza: “Tuko na Martha Karua ambaye ni imara na mwenye msimamo, Wycliffe Oparanya, Hassan Joho, Jeremiah Kioni na wanasiasa wengi vijana ambao wana uwezo wa kuongoza Azimio.”

Bw Odinga alisema yeye na viongozi wenzake wa Azimio hawawezi kuiacha nchini mikononi mwa Dkt Ruto na wenzake katika Kenya Kwanza ambao wameanza kupeleka nchini katika ule alioutaja kama “mkondo mbaya”.

“Kwa mfano wameanza kubuni upya tume nyingine ya uchaguzi pekee yao bila kuhusisha wadau wengi. Haja yao kuu kudhibiti IEBC kwa manufaa yao binafsi katika uchaguzi mkuu wa 2027,” akasema.

Kiongozi huyo wa ODM alisema haitakuwa na haja kwa mrengo wa Azimio kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao ikiwa mchakato wa kuundwa upya kwa IEBC haitashirikisha wahusika wote.

Kwa mara nyingine Bw Odinga alifafanua kuhusu madai kuwa mfichuzi alitoa ithibati ya kweli kwamba ni yeye (Raila) ndiye alishinda uchaguzi wa uraia kwa kura 8.1 milioni (asilimia 57) dhidi ya kura 5.9 milioni (asilimia 41) zake Rais Ruto.

Bw Odinga alishikilia kuwa matokeo ambayo mfichuzi huyo, anayesemekana kuwa mfanyakazi wa IEBC, yalitokana na takwimu za kura zilizonakiliwa kwenye sava za tume hiyo.

“Ukweli utajulikana hata zaidi ikiwa sava za IEBC zitafunguliwa. Hii ni kwa sababu hesabu zilizoko katika sava haziwezi kubadilishwa na hata kama matokeo yatabadilisha ushahidi utaonekana,” akasema.

Bw Odinga alisema kuwa uchakato wa upigaji kura uliendelea vizuri; kuanzia hatua ya upigaji kura, kuhesabiwa kwa kura katika vituo vya kupigia kura na ujumuishaji wa kura katika ngazi ya maeneo bunge.

Alisema hitilafu zilizotokea katika kituo cha kujumuisha kura za urais katia ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi anadai hesabu za kura zilivurugwa ili kumfaidi Rais Ruto.

“Shida hasa ilikuwa kutangazwa kwa matokeo katika Kituo cha Kitaifa cha Ujumlishaji katika Bomas. Hapo ndipo palikuwa na shida na tulieleza hayo kila wakati. Hatukufurahiswa na kilichokuwa kikifanyika na tulijaribu kumweleza mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati na timu yake,” Bw Odinga akasema.

Hata hivyo, Bw Odinga aliungama kuwa kambi yake haikuwa na maajenti katika vituo vyote 46,000 vya kupigia kura kote nchini.

Aidha, alisema maajenti wake waliokuwa katika ngome za aliyekuwa mpinzani wake mkuu, Rais Ruto, hawakuruhusiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura.

“Haikuwezekana kwa sisi kama Azimio kuwa na maajenti katika vituo vyote vya kupigia kura nchini. Na katika ngome za wapinzani wetu haswa katika Mlima Kenya maajenti wetu walidhulumiwa, kushambuliwa na hata kuzuiwa kuingia vituoni,” Bw Odinga akasema.

Akiongea katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi, Rais Ruto alitangaza kuwa Azimio haitamtambua Dkt Ruto Rais pamoja na maafisa wote wanaohudumu chini yake.

  • Tags

You can share this post!

Mamake Koigi wa Wamwere kufidiwa Sh2.5 milioni

KCB wamwaga Sh5 milioni kwenye gofu ya wanawake ya Magical...

T L