• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Ruto ameingia baridi – Mucheru

Ruto ameingia baridi – Mucheru

ONYANGO K’ONYANGO Na SILAS APOLLO

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia (ICT) Joe Mucheru jana Ijumaa alishambulia Naibu wa Rais William Ruto kufuatia madai kuwa wizara yake inapanga kuiba kura za urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Bw Mucheru alisema kuwa madai hayo ni ishara kwamba Dkt Ruto ameanza kuingiwa na hofu ya kushindwa katika uchaguzi ujao.

Dkt Ruto Alhamisi sekretariati ya kampeni za Dkt Ruto ilidai ilisema kuwa hatua ya Waziri Mucheru kutangaza kumuunga mkono mwaniaji wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ilikuwa ishara kwamba alilenga kutumia wadhifa wake kuiba kura.

Sekretariati hiyo inayoongozwa na Gavana wa Turkana Josphat Nanok, ilisema kuwa wizara ya ICT inahusika pakubwa katika upeperushaji wa matokeo hivyo ni hatari kwa waziri kuegemea mrengo fulani wa kisiasa.

“Wizara ya ICT ndiyo inasimamia Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA). CA inahusika na maandalizi ya miundomsingi ya kidijitali itakayotumiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kupeperusha matokeo,” akasema Bw Nanok.

Mrengo wa Ruto ulitoa malalamishi siku moja baada ya Bw Mucheru na waziri wa Afya Mutahi Kagwe kujitokeza na kuunga mkono Bw Odinga walipokuwa katika Kaunti ya Nyeri, Jumatano.

Lakini Bw Mucheru alipuuzilia mbali madai hayo ya mrengo wa Naibu wa Rais akisema kuwa ni propaganda inayolenga kumchafulia sifa.

“Nimesikia watu wakinishutumu kwa kuunga mkono Bw Odinga. Wanataka tume ya IEBC isinijumuishe katika maandalizi ya uchaguzi. Kura za maoni za hivi karibuni zinaonyesha kuwa mambo ni mabaya kwao sasa wanatafuta sababu ya kunilaumu endapo watabwagwa katika Uchaguzi Mkuu ujao,” akasema Bw Mucheru.

Waziri huyo alisema kuwa ni haki yake ya kikatiba kuegema mrengo wa kisiasa anaotaka huku akishikilia kuwa uhusiano wake na Bw Odinga hautaathiri majukumu yake ya uwaziri.

Bw Mucheru pia alikosoa Dkt Ruto kwa kutumia rasilimali za serikali kufanyia kampeni zake za kibinafsi badala ya kuhudumia wananchi.

Wakati huohuo, Dkt Ruto ametupilia mbali mpango wake wa kutengeneza kituo cha kuhesabia kura katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Awali, chama cha UDA kilikuwa kimesema kuwa kitaweka kituo sambamba cha kujumulisha matokeo sawa.

Inaonekana viongozi wa UDA wanahofia kupatwa na masaibu sawa na yale yaliyokumba muungano wa NASA katika uchaguzi wa 2017 ambapo watu waliodaiwa kuwa maafisa wa polisi walivamia kituo cha kujumulisha matokeo mtaani Westalands, Nairobi, siku tatu kabla ya uchaguzi na kuharibu mitambo.

Wataalamu wa kigeni John Aristotle Philips (Mwamerika), Andreas Katsouris ambaye ni raia wa Canada na raia wawili wa Ghana walioletwa na Bw Odinga kusimamia kituo hicho cha kujumulisha matokeo walirejeshwa makwao kwa nguvu na serikali.

Ijumaa, muungano wa Kenya Kwanza unaojumisha chama cha UDA, ulisema kuwa utategemea maajenti kulinda kura zake.

Msimamizi wakampeni za Dkt Ruto, Josphat Nanok alisema kuwa watahakikisha kuwa UDA itakuwa na maajenti wanaoaminika katika vituo vyote nchini.

“Hatuna mipango ya kuanzisha kituo mbadala cha kuhesabia kura. Kikatiba, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ndiyo inafaa kujumlisha na kutangaza matokeo rasmi,” akasema Gavana Nanok.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inakadiria kuwa nchi inaweza kuwa na vituo 53,000 vya kupigia kura, kutoka 40,883 mwaka wa 2017.

Wakati wa uchaguzi, wagombea urais wanatakiwa kuwa na angalau wakala mmoja kwa kila kituo cha kupigia kura.

Mbunge wa Kimilili, Didmus Barasa pia alisema kuwa watalinda kura zao mashinani hadi mshindi atakapotangazwa.

“Maajenti wetu hawataondoka katika vituo vya kupigia kura kabla, wakati au baada ya kupiga kura. Watakaa kote, hadi hesabu itakapokamilika,” akasema Bw Barasa.

Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Johnstone Muthama, aliambia Taifa Leo kuwa watategemea maajenti kupata matokeo yao katika vituo mbalimbali vya kupigia kura kote nchini.

  • Tags

You can share this post!

Sonko aanza ngoma Mombasa

Wito wazazi wakome kutumia kauli ya Magoha kuhepa kulipa...

T L