• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Talaka ya NASA yakamilika sasa chama cha ODM kikijiondoa

Talaka ya NASA yakamilika sasa chama cha ODM kikijiondoa

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, nacho kimeamua kujiondoa katika muungano wa National Super Alliance (NASA).

Katika hatua inayoashiria kuibuka kwa miungano mipana mipya, chama hicho kimesema kimeamua kushirikiana na vyama vingine kubuni muungano mpya kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya washirika wake katika NASA, Wiper cha aliyekuwa makamu rais Kalonzo Musyoka, Amani National Congress (ANC) cha aliyekuwa Naibu waziri mkuu Musalia Mudavadi na Ford Kenya cha Seneta wa Bungoma Moses Wetangula, kuamua kujiondoa katika muungano huo vikilaumu ODM kwa usaliti.

Watatu hao walisema kwamba wataungana chini ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ambao pia umekumbwa na hatari ya kutibuka baada ya chama cha Kanu kukataa kujiunga nao kikisisitiza kwamba hakitavunja ushirika wake na chama cha Jubilee.

Alhamisi, Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama cha ODM liliamua kwamba chama hicho kijiondoe katika muungano huo na kusaka washirika wapya kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

“Baraza Kuu la Kitaifa la chama cha ODM limepitisha kuwa chama cha ODM kitajiondoa katika muungano wa NASA. Kufuatia uamuzi huu, chama kitaandikia msajili wa vyama vya kisiasa kumfahamisha uamuzi huo,” alisema Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna baada ya mkutano wa NEC katika hoteli ya Kempinski jijini Nairobi.

Bw Sifuna alisisitiza kuwa uhusiano wa ODM na vyama tanzu vya muungano wa NASA ulifikia kikomo Januari 30 2018, Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula walipokataa kuhudhuria hafla ya kujiapisha kwa Bw Odinga kuwa rais wa wananchi katika bustani ya Uhuru Park Nairobi.

“Kwetu, NASA imekuwa historia. Wenzetu walitusaliti waliposusia hafla ya kuapisha kiongozi wa chama chetu Uhuru Park,” alisema.

Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula wamekataa kumuunga mkono Bw Odinga kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Matumaini yao yamekuwa katika muungano wa OKA ambao wamekuwa wakisuka pamoja na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi ambaye chama chake kimekataa kuvunja ushirika wake na chama cha Jubilee. ODM, pia kimekuwa kikisuka muungano na Jubilee lakini mchakato huo ulisitishwa baada ya chama hicho tawala kukumbwa na msukosuko wa ndani.

Vinara wa OKA wamekuwa wakikaribisha ODM kujiunga na muungano huo hatua ambayo Bw Sifuna anasema hawaikumbatii kwa sasa.

“Tunatafuta marafiki wapya. Kuna takriban vyama 100 vya kisiasa nchini na tunalenga kuzungumza na vilivyo na malengo sawa na ODM,” alisema.

Duru zinasema kuwa ODM kiko makini kufanikisha muungano na Jubilee ambao unahusisha Kanu na vyama vingine vilivyounga Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Bw Sifuna alisema licha ya kuamua kujiondoa NASA, ODM kitagawia washirika wake katika muungano huo pesa kinazopata kutoka hazina ya vyama vya kisiasa kama kiinua mgongo tu na si kwa sababu ya mkataba wao.

“Kiongozi wetu amekubali kwa roho safi kuwapa washirika wetu kiinua mgongo ikizingatiwa tumekuwa na baadhi yao tangu 2013. Tutafanya hivyo si kwa sababu ya mkataba wa NASA lakini kwa nia njema tu,” alisema Bw Sifuna.

Kujiondoa kwa ODM katika NASA kutaua rasmi muungano iwapo Wiper na ANC vitaandikia rasmi msajili wa vyama kujiondoa.

You can share this post!

Makarios na DN Hotstars zatiga robo fainali Dennis Oliech...

UIGIZAJI: Lynn aamini hatua moja baada ya nyingine...