• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Tatueni shida za wananchi badala kunilaumu, Uhuru aambia naibu rais

Tatueni shida za wananchi badala kunilaumu, Uhuru aambia naibu rais

NA WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta mnamo Jumatano alimtaka Naibu Rais William Ruto kubuni suluhisho kwa changamoto zinazowakumba Wakenya, badala ya kulalamika kila mara na kuilaumu serikali.

Akihutubu jijini Mombasa kwenye Kongamano la Kila Mwaka la Walimu Wakuu wa Shule za Upili, Rais alisema ni kinaya kwa viongozi kulalamika wakati wanaangaliwa na wananchi kutoa suluhisho kwao.

“Viongozi wanapaswa kukoma kulialia na badala yake kuwa jibu kwa matatizo yanayowaandama raia. Unawasaidia vipi unapoanza kulalamika kama wao ilhali unafaa kuwasaidia?” akashangaa Rais Kenyatta, kwenye kauli iliyomlenga Dkt Ruto.

Katika siku za hivi karibuni, Dkt Ruto amekuwa akiikosoa serikali kutokana na changamoto zinazowaathiri Wakenya, baadhi yazo zikiwa uhaba wa mafuta na kupanda kwa gharama ya maisha.

Wiki iliyopita, Dkt Ruto aliilaumu serikali kwa kusababisha uhaba wa mafuta kimakusudi na kupuuza changamoto zinazowakumba.Dkt Ruto alitaja hali hiyo kuchangiwa na “maafisa wakuu wa serikali wasiowajibika hata kidogo.”

“Hali ilivyo sasa ni dhihirisho kuwa, kuna makundi hatari ambayo yameanza kungilia na kudhibiti kila sekya ya uchumi wetu. Wakenya wanataka kukomesha hali hii. Mtindo wa serikali kupuuza changamoto za mamilioni ya Wakenya ndio unaoneana makundi hayo ushujaa,” akasema Dkt Ruto, alipohutubu Jumatatu wiki iliyopita.

Akaongeza: “Ndiyo sababu hata wakati tunapokumbwa na changamoto hizi, maafisa wakuu wa serikali wanaonekana kutojali hata kidogo, bali masuala wanayoyapa kipao mbele ni Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) na siaza za mrengo wa Azimio.”

Ikiwa hotuba yake ya mwisho kwa walimu wakuu hao kabla ya kung’atuka uongozini Agosti, Rais Kenyatta alisifia hatua zilizochukuliwa na serikali yake kuboresha sekta ya elimu nchini.

Walimu pia walifurahia “ukarimu” wa Rais Kenyatta baada ya kuahidi kuwanunulia chakula cha mchana.

“Ninapata shinikizo kuwanunulia chakula cha mchana, japo hilo jukumu nitamwachia Gavana Hassan Joho,” akasema Rais huku akishangiliwa na walimu hao.

Alisema kutokana na mpango uliowekwa na serikali kuhakikisha kila mwanafunzi anayemaliza shule ya msingi anajiunga na shule ya upili, idadi ya wanafunzi katika shule za upili imeongezeka kutoka 1.3 milioni mnamo 2018 hadi 3.6 milioni mwaka huu.

Alieleza kuwa chini ya mpango huo, zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi wanaofanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) huwa wanajiunga na shule za upili.

Vile vile, alieleza kwamba serikali iko kwenye hatua za mwisho mwisho kumaliza ujenzi wa madarasa 10,000 ya kuendeshea Mpango wa Elimu ya Umilisi na Utendaji (CBC).

“Kufikia sasa, tumejenga jumla ya madarasa 6,470. Madarasa yaliyobaki yatajengwa kwenye awamu ya pili ya mpango huo,” akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Ushuru wa VAT, PAYE usitishwe – Wanaharakati

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa limbukeni nchini...

T L